Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa jana alikuwa kivutio kwa wananchi katika sherehe za kuapishwa Rais Dk John Magufuli, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana kwake hadharani tangu azushiwe kifo mtandaoni.
Juzi, kulikuwa na ujumbe uliokuwa unasambaa kwenye mitandao ya kijamii ukidai kuwa amefariki dunia ambao hata hivyo baada ya habari hizo kusambaa, Idara ya Habari (Maelezo), ilikanusha taarifa hizo ikisema ni mzima wa afya na hasumbuliwi na maradhi yoyote.
Katika sherehe hizo za jana, baada ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuingia uwanjani hapo saa 3.04 asubuhi na mshereheshaji, Sued Mwinyi kutangaza; “anayefuata ni Rais Mstaafu, wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa,” wananchi walilipuka kwa hoihoi, nderemo na vifijo kumshangilia.
Wakati akishangiliwa, Mkapa mwenyewe ambaye aliingia uwanjani hapo saa 3.05 akiwa amevalia suti nyeusi, alielekea moja kwa moja jukwaani huku akitabasamu.
Mbali na Mkapa, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alishangiliwa kwa nguvu wakati alipokuwa akisalimiana na Rais Magufuli. Baada ya kuapishwa, kukagua gwaride na kupigiwa mizinga 21 alielekea jukwaa kuu ambako kabla ya kuketi, alisalimiana na viongozi mbalimbali na ilipofika zamu ya Rais Kagame umati wa watu ulishangilia kwa nguvu hali iliyosababisha Rais Magufuli awanyoshee mikono miwili wananchi kama ishara ya kuwasalimia.
Akizungumzia kitendo hicho, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema Rais Kagame amekuwa msimamizi wa ukuzaji wa uchumi katika nchi yake. “Ameitoa nchi hiyo katika vita lakini na sasa Rwanda inakua kwa kasi kiuchumi, wananchi wanafuatilia, inawezekana ndiyo maana wamemshangilia.”
Maoni ya wananchi
Wakizungumza uwanjani hapo, mwanachama wa ACT – Wazalendo, Justina Mosha, alisema amefurahishwa na hotuba ya Dk Magufuli hasa alipowataka wanasiasa kuondoa tofauti za kiitikadi na kujenga Tanzania.
“Ni kweli tumetumia muda mwingi kwenye majukwaa sasa kilichobaki kuijenga Tanzania kiuchumi,” alisema.
Mwenyekiti wa Chaumma, Tawi la Charambe, Hussein Mlaponi alisema hotuba ya Magufuli imeonyesha ukomavu wa kisiasa hasa baada ya kuahidi kushirikiana na vyama vya upinzani.
“Nimefurahi Rais amesema hao siyo wapinzani, bali ni washindani wake kisiasa na atashirikiana nao,” alisema.
Damian Komba wa Temeke alimshauri Rais Magufuli aunde baraza dogo la mawaziri ili kupunguza gharama za uendeshaji. “Alishaahidi kwenye kampeni zake kwamba atakuwa na baraza dogo la mawaziri, sasa tunasubiri utekelezaji wake.”
Amina Maige wa Mwananyamala alisema matarajio ya wengi ni kwamba atatekeleza mambo yote aliyoyaahidi hasa kuboresha uchumi wa mtu mmojammoja.
“Hivi saa watu wana hali ngumu ya maisha kiasi kwamba wengine wanakula mlo mmoja kwa siku, atutoe kwenye umaskini huo,” alisema.
Alisema bidhaa hasa vyakula vipunguzwe bei pamoja na kupata huduma za afya zenye uhakika.
Mkazi wa Gongolamboto, Hamis Athumani Chamkali alimwomba Rais Magufuli kuendelea na mchakato ya Katiba Mpya ulioachwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Arusha
Akizungumzia kuapishwa kwa Rais Magufuli jana, mfanyabiashara wa utalii, Mathew Mollel alisema pamoja na kuapishwa kwake, hali ya Zanzibar inampa hofu.
Alisema Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hali ya wasiwasi na hatua ya uchaguzi kufutwa kisiwani humo inamtia hofu.
Mkazi mwingine wa Sakina, Vivian Mtei alisema anajisikia vibaya kuapishwa kwa Rais Magufuli kwa kuwa anahisi uchaguzi haukuwa wa huru na haki.
-MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment