Wagombea wanne urais wa Zanzibar wametaka kufutwa kwa uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na kufunguliwa mashtaka kutokana na kitendo chake cha kujitangaza ameshinda urais kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kutangaza matokeo.
Wagombea hao walitoa tamko hilo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari, Vuga, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wenzake,
mgombea wa urais kupitia chama cha AFP, Soud Said Soud, alisema kitendo
cha Maalim Seif kujitangaza kuwa mshindi katika uchaguzi huo kabla ya
Zec ni kinyume cha sheria ya uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984.
“Tunamshauri Rais wa Zanzibar kufuta
uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika
kipindi hiki cha mpito kutokana na kiongozi huyo kupoteza sifa za
kuendelea kushika wadhifa huo na nafasi hiyo apewe mtu mwingine,”
alisema Soud.
Alisema inashangaza kuona vyombo vya
sheria na Zec wanakuwa wazito kuchukua hatua za kisheria wakati ni kosa
kwa mgombea kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi ya tume hiyo.
“Hatua hiyo imeanza kujenga dhana
miongoni mwa wananchi kwamba sheria za nchi hii zimewekwa kwa watu
maalum na wengine wapo juu ya sheria hizo,” alisema mgombea huyo.
Aidha, alisema kauli na matamshi ya
Maalim Seif ambayo amekuwa akiyatao hadharani dhidi ya Rais wa Zanzibar
yanamuondolea sifa ya kuendelea kushika wadhifa huo akiwa mshauri mkuu
wa Rais katika kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa kifungu cha 39 (5) cha
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Wagombea hao wameunga mkono uamuzi wa
Mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanziba uliofanyika
Oktoba 25, mwaka huu.
Wagombea waliotoa tamko hilo ni, Ali
Khatibu Ali (CCK), Hafidhi Hassan Suleiman (TLP) na Issa Mohamed Zonga
ambao wamesema wanasubiri taarifa ya siku ya kufanyika uchaguzi
mwingine.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment