Baada ya Chama cha Haki Miliki Tanzania (COSOTA) pamoja na kampuni ya kusimania haki miliki za wasanii, Copyrights Management East Africa Limited
(CMEA) kutangaza neema kwa wasanii kuanza kunufaika kwa kulipwa
mirahaba itokanayo na kazi zao kuchezwa kwenye redio na TV, wasanii
wachanga wameanza kuwa na hofu na mfumo huo.
Akizungumza na 255 ya XXL kupitia Clouds FM, Afisa Mtendaji Mkuu
COSOTA, Doreen Anthony alisema kila kazi ya msanii itakayosikika
itatakiwa kulipiwa.
“Kwetu sisi tunaona kwamba hii ni biashara, muziki ni biashara na
redio na TV ni biashara,” alisema. “Ili wote tuweze kufaidika, msanii,
TV na redio pamoja na serikali ifaidike, kwanini mtu aseme basi nisipige
wimbo wa mtu ambaye anachipukia kwaajili tu ya kumkomoa ili ulisilipe?
Piga mlipe achukue chake na wewe uchukue chako maisha yaendelee.”
alisisitiza.
Kwa upande wa mkurugenzi mkuu wa CMEA, Paul Matthysse aka P-Funk
alisema kila msanii anatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili anufaike na
kazi yake.
“Kitu kimoja unajua mfumo wetu wa Tanzania hakuna demo artist na
hakuna artist mkubwa, msanii mdogo ambaye alifanya demo anaweza naye
kupata airtime, nje ni ngumu hivyo,” alisema.
“Ndio maana talent inakuwa kwenye level ya hali ya juu, ukiwa bora
ndio utapata nafasi zaidi ya kutoka na kusikika. Usiwalaumu media,
tunachohitaji ni muziki uwe wa maana. Muziki mzuri wa kuvutia mashabiki
na wasikilizaji na upigwe. Waimbaji wazuri ambao wapo kwenye hali ya juu
ili tuweze kupandisha level ya muziki wetu. Kwa hiyo kaza buti, fanya
kazi na wewe ufike level inayohitajika, hakuna ubaguzi wala nini kazi
ikiwa nzuri ni nzuri.”
0 comments:
Post a Comment