Jeshi la Polisi Mkoani hapa
limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye Ismail Swalehe Sang’wa (20)
ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Sepuka wilayani Ikungi katika Mkoa wa
Singida kwa tuhuma za kumuua Afisa wa Intelijensia wa TANAPA aitwaye
Emily Kisamo (52).
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake asubuhi ya leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo la
mauaji ya Afisa huyo wa TANAPA lilitokea tarehe 18.12.2015 muda kati ya
saa 2:30 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi mtaa uitwao Corridor Area
Uzunguni jijini hapa.
Kamanda Sabas alisema kwamba,
siku ya tukio hilo marehemu alikuwa nyumbani kwake sebuleni akiwa
anakunywa uji ndipo mtuhumiwa ambaye ni mfanyakazi wake wa ndani na
alimvizia na kumkata shingo na kitu kinachoaminika kuwa ni panga na
kisha kuchukua mwili wake na kuuweka kwenye gari la marehemu aina ya
Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY.
“Baada ya kuuweka mwili wa
marehemu kwenye buti alilisafisha gari hilo kwa nje na kisha kuliendesha
mpaka eneo la kikwakwaru “B” kata ya Lemara ambapo alilitelekeza hapo
na kisha yeye kuondoka”. Alifafanua Kamanda Sabas.
“Mara baada ya gari hilo kukaa
mpaka saa 2:00 usiku ndipo baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitoa
taarifa kwetu ambapo askari wa doria walikwenda na kulichukua gari hilo
kwa kulivuta mpaka kituoni. Kwa kuwa mke wa marehemu aitwaye Caroline
Lukumay (38) alikuwa anamtafuta mume wake kwa njia ya simu bila
mafanikio ndipo alipoamua kuja kituoni kutoa taarifa ambapo
tulimuonyesha gari lililotelekezwa ambalo alillitambua mara moja”.
Alisema Kamanda Sabas.
Aliongeza kwa kusema kwamba
askari walimuomba mke wa marehemu funguo za akiba za gari hilo ambapo
baada ya kulifungua ndipo walipouona mwili wa marehemu kwenye buti akiwa
na vitu mbalimbali kama vile simu mbili aina ya Sony na Panasonic, pesa
taslimu Tsh 300,000, Laptop aina ya Asus na kadi za benki tofauti
tofauti.
Mara baada ya mtuhumiwa huyo
kukamatwa alikiri kuhusika na mauaji hayo na kusema siku hiyo walikuwa
wawili tu yaani yeye na mrehemu na alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa na
tamaa za fedha alizokuwa nazo marehemu ndani ya nyumba hiyo kiasi cha
Tsh. Mil.5.
Upekuzi zaidi wa Jeshi la
Polisi ulibaini kuwepo kwa fedha taslimu Tsh. 4,294,000, simu tatu aina
ya Sumsang na vocha za mtandao wa vodacom za sh. Elfu tano tano zenye
thamani ya Tsh. 70,000 ambapo vyote vilifukiwa kwenye banda la kuku.
Mbali na vitu hivyo pia
mtuhumiwa Ismail Swalehe Sang’wa aliweza kuonyesha panga lenye damu
ambalo alilihifadhi stoo pamoja na taulo nne kubwa, kitambaa cha mezani
na suruali yake ambazo zilikuwa na damu na alizitumia yeye mwenyewe
kupigia deki sebuleni baada ya tukio na kisha kuzificha kwenye migomba
karibu na mabanda ya kuku.
Kamanda Sabas alimalizia kwa
kusema kwamba Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watatu wengine mbali
na Ismail Swalehe Sang’wa akiwemo mke wa marehemu, rafiki wa mke wa
marehemu ambaye ni mwanamke na dereva wa nyumbani wa marehemu kwa
mahojiano zaidi.

0 comments:
Post a Comment