Friday, December 18, 2015




KAMPUNI ya serikali inayotoa huduma za meli katika eneo la Maziwa Makuu, Marine Services Company Ltd (MSCL), inadaiwa kutumia kinyume sh.milioni 300 kati ya milioni 600 ilizokuwa imepewa kutengeneza meli ya Mv.Victoria.
 
Hali hiyo iligunduliwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza Magesa Mulongo baada ya kutembelea ofisi za kampuni hiyo zilizopo Bandari ya Mwanza Kaskazini.
 
Uongozi wa MSCL unadaiwa kutumia fedha hizo kulipa mishahara badala ya kutengeneza meli hiyo iliyojengwa mwaka 1964, ambayo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa imeegeshwa katika Bandari ya Mwanza Kusini, kutokana na kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kangavuke (Generator) ya kufua nishati ya umeme melini.
 
Hali hiyo imewaathiri vibaya abiria na wasafirishaji wa mizigo kati ya Mwanza na Bukoba.

Desemba mwaka jana Mv Victoria ilipandishwa kwenye chelezo ili ifanyiwe matengenezo,kazi iliyopaswa kuanza Julai mwaka huu, lakini haikufanyika kutokana na fedha kukosekana; hivyo ikashushwa kutoka kwenye chelezo.

Imedaiwa kuwa matengenezo ya meli hiyo inayotegemewa na wakazi wa Mikoa ya Mwanza na Kagera,yamekwama kutokana na kiasi cha fedha kutumika kulipa mishahara ya wafanyakazi na kiasi kingine kununua vipuri kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa meli nyingine (Mv.Serengeti) kinyume na maelekezo ya serikali.


0 comments:

Post a Comment