MAWAZIRI wawili jana ‘walitumbua majipu’ baada ya kutangaza
kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka
(DART), Asteria Mlambo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road, Dk Diwani Msemo, wote wakipisha uchunguzi dhidi yao.
Mlambo amesimamishwa kazi kuanzia jana ili kupisha uchunguzi baada ya
serikali kubaini ukiukwaji wa wazi wa Sheria ya Manunuzi ya Umma katika
kumpata mtoa huduma ya mpito wa mradi huo wenye nia ya kupunguza
msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na
usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George
Simbachawene alisema kutokana na kukamilika kwa sehemu ya ujenzi wa
miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali iliamua kuwa na mtoa
huduma wa mpito kabla ya kumpata wa kudumu.
“Mtoa huduma wa mpito alipaswa kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya
Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa
sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa kipindi cha mpito.
“Kufuatia hali hiyo nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23
Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha
uchunguzi,” alieleza Simbachawene.
Simbachawene alizitaja sababu za kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu huyo
wa DART kuwa ni kushindwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati
wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito;
kushindwa kuchukua
hatua hata pale alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti
ya mkataba wa kutoa huduma ya mpito; na kufanya maamuzi makubwa pasipo
kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.
Aidha, alisema Serikali inatambua kuwa wapo watumishi wa DART ambao
hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu, hivyo watumishi hao watachunguzwa na
kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu atakayeteuliwa.
“Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi kuendelea na taratibu
za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi,” alisema
Simbachawene. Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua
hatua kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uanze kutoa huduma bora ya
usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam bila kuchelewa zaidi, huku akiwaomba
kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu fedha
nyingi kwa manufaa yao.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea maeneo ya
mradi huo wa DART na kuagiza kuwa uanze kazi Januari 10, mwakani baada
ya kupigwa kalenda kwa muda sasa tangu mwaka jana.
Wakati Simbachawene akichukua hatua hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemsimamisha Dk Msemo
kwa kile kilichoelezwa ni kupisha uchunguzi unaolenga kubaini iwapo
mgongano wa kimaslahi umeathiri utendaji wa taasisi hiyo.
Aidha, watendaji wote wa serikali katika sekta ya afya hususan wakuu
wa vituo vya kutolea huduma za afya, wafamasia, wauguzi na waganga
wafawidhi, wameagizwa kukiri kwa maandishi ndani ya siku 21 kuanzia sasa
endapo wanamiliki hospitali, zahanati, kliniki na maduka ya dawa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri Mwalimu,
imefafanua uamuzi wa kumsimamisha Kaimu Mkurugenzi huyo wa Ocean Road,
unatokana na ziara walizofanya kukagua utoaji wa huduma za afya katika
maeneo mbalimbali ambako walibaini upungufu wa dawa umeendelea
kujitokeza kwa wingi.
“Baadhi ya wagonjwa walieleza kwa uchungu jinsi wanavyopata tabu ya
kupata dawa hata zile ambazo wanatakiwa wazipate kwa bei ya ruzuku au
zinazotakiwa kutolewa bure na serikali,” ilisema taarifa hiyo.
“Kwa kuzingatia suala hili la mgongano wa kimaslahi, manung’uniko
mengi kutoka kwa wapokea huduma, hususan katika Taasisi yetu ya Saratani
ya Ocean Road, nimechukua hatua ya kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi,”
iliongeza taarifa ya waziri huyo.

0 comments:
Post a Comment