SERIKALI imesisitiza azma yake ya kufanya mabadiliko ya watendaji wa
Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kufuatia kushamiri kwa urasimu na
kukosa ubunifu.
Imesema hatua hiyo imetokana na baadhi yao kukosa ubunifu katika
uanzishaji na uendelezaji wa miradi ya umeme na kusababisha majadiliano
ya mikataba ya uzalishaji umeme kuchukua muda mrefu.
Aidha, ilisema kwa vyovyote gharama za umeme lazima zipungue, hivyo
imeziagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na
TANESCO kuwasilisha mapendekezo kupitia upya gharama hizo.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, alitoa wito kwa watu na taasisi binafsi nchini kwenye
uzalishaji umeme ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika na wa
gharama nafuu.
Profesa Muhongo aliyasema hayo wakati wajumbe wanaounda Shirikisho la
Viwanda Tanzania (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na
Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) walipofi ka
kuwasilisha changamoto mbalimbali za umeme wanazozipata katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema serikali inakaribisha wawekezaji wazalishe umeme kwenye
miradi midogo ya maji isiyozidi megawati 10 ambayo itasadia wananchi
walio nje ya gridi ya taifa kupata umeme.
Aliitaja miradi mingine ambayo wawekezaji wana fursa ya kuwekeza kuwa
ni uzalishaji umeme kwa kutumia nguvu ya upepo, jua, jotoardhi,
mawimbi, tungamotaka, na bayogesi.
Alielezea lengo la serikali la kutaka kuzalisha umeme kwa kutumia
makaa ya mawe ambapo kuna tani zaidi ya bilioni 9 ambako alizialika
tasisi hizo binafsi kushirikiana na serikali kwenye uzalishaji huo.

0 comments:
Post a Comment