Rais Dk. John Magufuli, amekutana na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad pamoja na Mkurugenzi wa
Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Eutropius Mganga, Ikulu jijini Dar es
Salaam na kuwapa mambo matatu muhimu anayoyataka katika serikali yake ya
'Hapa kazi tu'.
Pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, wamezungumzia mambo mbalimbali
kuhusu mustakabali wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Akizungumzia yaliyojiri katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, Prof.
Assad alisema kwanza walizungumzia kupunguza gharama za matumizi ya
kuendesha serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Profesa Assad alibainisha kuwa Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ihakikishe Tanzania inaongeza
ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya pato la Taifa (GDP) kwa
mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.
"Hadi mwaka juzi Tanzania ilikua inakusanya mapato kwa kiwango cha
asilimia 14 ya pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikua
ikikusanya asilimia 19 ya pato Taifa, na hakuna sababu za msingi za kwa
nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo," alifafanua
Prof. Assad.
Wakati Ofisi ya GAG ikitakitakiwa kufanya mambo hayo mawili, jambo la
tatu lilielekezwa kwa DPP, Mganga ambaye alisema mazungumzo yao
yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya
serikali ya awamu ya tano isemayo "Hapa Kazi Tu"
Aidha, Mganga ameongeza kuwa wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza
Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake
bila kumuonea mtu.
Kiongozi mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mufti Mkuu wa
Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Ally, ambaye pamoja na kumpongeza rais
kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema Waislamu
wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili
aendelee na juhudi hizo.
"Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka kumueleza kwamba kazi anayoifanya
ni kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba aendelee kuifanya wala
asiogope, na kauli yake ya 'Hapa Kazi Tu' iendelee, kwa sababu
inaonyesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri," alibainisha
Mufti Mkuu,
Kadhalika, rais alikutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Alhaji Abdallah Bulembo, ambaye alimpongeza kwa
kasi nzuri aliyoanza nayo katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2015- 2020 na kutaka kasi hiyo iendelee.
Alisema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayoifanya na kwamba
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi
katika kutekeleza Ilani ya CCM.
"Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza
kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na
hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada," alisisitiza
Alhaji Bulembo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment