
Katika
kile kinachoonekana kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John
Magufuli haitalegeza kamba linapokuja suala la kusitisha safari holela
za nje za watumishi wa umma, Idara ya Uhamiaji imesema
bado inakagua uwapo wa barua ya mwajiri na kibali maalum cha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Awali, ili kusafiri nje ya nchi mtumishi wa umma alihitaji pasi ya kusafiria yenye viza na tiketi.
Akizungumza
na Nipashe kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile,
Msemaji wa Idara hiyo Tabu Burhan, alisema idara hiyo inaendelea
kusimamia kikamilifu maelekezo ya Rais.
Katika
utekelezaji wa agizo hilo, kila mtumishi wa umma anayesafiri nje ya
nchi anatakiwa kuonyesha barua ya mwajiri wake na kibali cha Ikulu,
alisema.
Burhani
alisema Idara hiyo inafanya ukaguzi huo katika vituo vya usafiri kama
viwanja vya ndege na mipakani ili kubaini watu watakaokiuka kwa makusudi
agizo la Rais Magufuli.
Burhan
alisema ingawa kazi ya kuwadhibiti watumishi wa umma wanaosafiri nje ni
ngumu kutokana na hati zao za kusafiria kutoonyesha kazi wanazofanya,
lakini wamejipanga vizuri kutumia mbinu mbalimbali kuwabaini.
“Tutawabana
wakija kugonga mihuri hati za kusafiria, tukigundua ni mfanyakazi wa
serikali tutamuomba atupatie barua kutoka kwa mwajiri na kibali cha
Ikulu, kama hana tunamrudisha na hataweza kusafiri,” alisema Burhan.
Alisema
zamani ilikuwa rahisi kwa kila mtumishi aliyetaka kusafiri nje ya nchi
kutambulika kazi yake kwasababu walikuwa wakitakiwa kujaza fomu iitwayo
TIF 10 na TIF 12, mfumo ambao ulisitishwa mwaka 2005 baada ya kuanza
kutumika hati za kusafiria za kieletroniki.
“Tunawashauri
watumishi ambao wanataka kusafiri wajiridhishe wenyewe kwanza, itakuwa
usumbufu na hasara endapo tutawarusidisha wakiwa tayari uwanja wa
ndege,” aliongeza.
Akizungumzia
idadi ya watu waliozuiliwa tangu kuanza kwa utekelezaji wake, msemaji
huyo alisema mpaka sasa hakuna mtumishi aliyenaswa mbali na wafanyakazi
wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ambao tayari
wamesimamishwa kazi.
Watumishi hao ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.
Agizo
la kuwazuia watumishi kusafiri nje lilitolewa na Rais Magufuli siku
moja baada ya kuapishwa kwa lengo la kubana matumizi ya serikali na hadi
sasa ameshaokoa mabilioni ya fedha.
Akilihutubia
Bunge la 11 na kulizindua mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli
aliwataka watanzania na wabunge waunge mkono uamuzi wake wa kupiga
marufuku safari za nje ambapo fedha nyingi zitaokolewa na kutumika
kwenye huduma za jamii kama barabara, afya na elimu.
Alitoa
mfano kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2013 na nusu ya 2014/2015
pekee, safari za vigogo nje ya nchi ziligharimu Sh. bilioni 356.3 fedha
ambazo alisema zingeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilomita 400 au
kutimiza miradi mbalimbali ya jamii.
Alisema
tiketi za ndege pekee ziligharimu Sh. bilioni 183.160, mafunzo ya nje
ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu Sh. bilioni 104.552.
Novemba
mwaka jana, Ikulu ilisambaza mwongozo unaoweka masharti ambayo
watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kuyatimiza
ili wapewe kibali cha kusafiri.
Sharti
la kwanza ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue na maombi yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda kwa
Sefue ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa safari hiyo na
tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Sharti
lingine linamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama taasisi apime kama
safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kabla ya
kuwasilishwa Hazina na aeleze manufaa ambayo nchi itapata kutokana na
safari hiyo.
Pia
sharti lingine linataka mhusika aeleze umuhimu wa safari hiyo na
isipofanyika itaathiri vipi nchi. Mwombaji aanatakiwa aeleze manufaa ya
safari hiyo kwa taasisi na taifa; kama imewahi kufanyika huko nyuma
ilisaidia nini.
Ofisi
za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba 12 mwaka
jana ikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje
ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake. Barua hiyo ya
Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment