Wasomi nchini wamekosoa hatua ya baadhi ya mawaziri kuwasimamisha kazi watendaji wa Serikali kutokana na sababu mbalimbali wakisema si dawa ya kurejesha utumishi uliotukuka bali kinachotakiwa ni kuweka mfumo imara wa utawala.
Katika
mahojiano na Mwananchi, wasomi hao wamesema baadhi ya mawaziri
wanachukua hatua hizo ili waonekane wachapa kazi lakini ukweli
wanachukua uamuzi bila kuwasikiliza wahusika, kufanya utafiti wa kina
wala kujua changamoto zinazowakabili.
Tangu
walipoapishwa Desemba 23, 2015, baadhi ya mawaziri wamekuwa wakifanya
ziara za kushtukiza, kutoa matamko na maagizo kwa watendaji wa Serikali,
ambapo mpaka sasa zaidi ya watendaji 20 wa Serikali, mashirika na
taasisi zake wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Baadhi ya
waliosimamishwa ni Ofisa Biashara Manispaa ya Ilala, Dennis Mrema
kutokana na agizo lililotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –
Tamisemi, George Simbachawene Januari 7, baada ya kutuhumiwa kusababisha
upotevu wa mapato kwa Serikali.
Januari
5, Waziri wa Masiliasi na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango wa Matumizi Endelevu ya
Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),
Mohammed Kilongo na maofisa misitu wa mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi
wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Pia,
Rais John Magufuli katika siku 70 za utawala wake ameshawatimua kazi
wafanyakazi 70 wakiwamo watumishi na wajumbe wa bodi wa mashirika au
taasisi husika wakidaiwa ama kushindwa kuwajibika au kutosimamia vizuri
maeneo yao.
Walioangukiwa
na rungu la Rais Magufuli ni watumishi na viongozi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Wizara ya Uchukuzi na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mhadhiri
wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Mohamed Bakari alisema kama hakutafanyika mabadiliko katika
mifumo ya uendeshaji katika taasisi na ofisi mbalimbali za umma
hakutakuwa na mabadiliko ya maana yatakayofanywa na mawaziri hao.
Bakari
alitolea mfano utendaji wa Mamlaka ya Bandari na TRA, akisema mfumo wa
utendaji ni ule ule, hivyo hata akiwekwa ‘mtendaji aliyetukuka’ mambo
yanaweza kuwa yaleyale kwa sababu utaratibu wa uendeshaji wa bandari
umeachwa kama ulivyokuwa awali.
Kuhusu
sakata la makontena kupitishwa bandarini bila kulipiwa kodi na tozo
mbalimbali, Bakari alisema wengi wanaopitisha mizigo ni wanasiasa, jambo
ambalo huwafanya wafanyakazi wa bandari kuwa wepesi wa kukubali mizigo
hiyo kupita bila kulipiwa chochote kwa kuhofia usalama wa kibarua chao.
“Kuwawajibisha
ni sawa, sasa tujiulize kuna mabadiliko ya mfumo ili kuwatengenezea
mazingira ya kufanya kazi bila kuingiliwa na mtu?” alihoji Bakari.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP), Lilian Liundi alisema
kabla ya kwenda mahali popote penye tatizo na kutoa tamko au kusimamisha
watu kazi, mawaziri wanatakiwa kufanya utafiti wa kina ili
kujiridhisha.
Alisema
wanachofanya hakina tatizo iwapo tu kitafanywa kwa haki kulingana na
ushahidi na vithibitisho walivyonavyo ili kuchukua uamuzi ambao
hautalalamikiwa na wahusika.
Alisema
licha ya kuwa watumishi wengi wa umma walifanya kazi kwa mazoea, kuna
njia nyingi za kurejesha utumishi bora, si lazima watu kusimamishwa kazi
au kufukuzwa.
“Kama
utafiti utafanyika na kubainika ukweli waadhibiwe tu, hapo hakuna
majadala kwa sababu uzalendo, uwajibikaji, kujituma kulipotea kabisa.
Watumishi wa umma walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea, hiyo inaweza kuwa
ndiyo sababu kubwa ya haya yanayotokea sasa, ” alisema Liundi.
Mkurugenzi
wa utetezi na maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Harold Sungusia alisema kinachoendelea sasa ni aina mbili za
uwajibishwaji. Kwanza ni ule aliosema hana shaka nao ambao ni wahusika
kuwajibishwa kwa makosa waliyoyafanya kwa bahati mbaya au makusudi.
Pili,
alisema ni uwajibishwaji unaohusisha visasi vya kisiasa au binafsi.
“Yaani mwenye nafasi au cheo hutumia nafasi hiyo kumwadhibu mwenzake
hata kama hana hatia kwa sababu tu ana uwezo wa kufanya hivyo, huo ndiyo
wenye shida.” Alisema pamoja na viongozi kuwa na haki kisheria ya
kuwaadhibu wanaokiuka maadili ya utumishi, lakini kuna haki ya msingi
kwa kila anayetuhumiwa kujieleza au kujitetea.
Alisema
kisheria kumwadhibu mtu bila kumsikiliza hata kama kuna ushahidi wa
kutosha ni kosa, lazima apewe nafasi ya kujitetea kwa maelezo kuwa
pengine alikuwa na sababu za kufanya hicho alichokifanya.
Alisema
anaunga mkono juhudi zinazofanywa sasa kwa watumishi wa Serikali
kutokana na mazoea na uzembe uliokithiri huku akisisitiza kuwa kutoa
nafasi kuwasikiliza wahusika, kufanya uchunguzi wa jambo kabla ya kutoa
uamuzi, ni masuala ya msingi yanayopaswa kufanywa na mawaziri.
CHANZO : MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment