OFISA wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) mkoani
Dodoma, Emmanuel Meta (37) ameuawa kufuatia kipigo cha watu ambao mpaka
sasa hawajafahamika.
Hata hivyo Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku katika eneo la Area C manispaa ya Dodoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP), David Mnyambuga, Ofisa huyo wa PCCB alifariki dunia wakati
anapatiwa matibabu baada ya kupigwa na watu ambao hakuwafahamu.
Alisema mtoa taarifa wa awali wa tukio hilo, Athuman Mtengwa ambaye
pia ni mfanyakazi PCCB, mkazi wa Area “D” alieleza kuwa, Januari 20, saa
6:15 usiku akiwa nyumbani kwake alipigiwa simu na Emmanuel (marehemu)
ambaye ni mfanyakazi mwenzake pia ni rafiki yake wa karibu.
Alisema Meta alimweleza kuwa anaomba msaada wa kupelekwa hospitali
kutibiwa kwa kuwa amepigwa na watu wasiofahamika wakati akirudi nyumbani
kwake akitokea baa ya Rose Garden iliyopo Area “C” jirani na nyumbani
kwake kwa matembezi.
Baada ya Mtengwa kufika alipiga honi ndipo Meta alitoka nje na
kufunga mlango na geti kwa kufuli na kuingia katika gari kuelekea
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wakiwa njiani hali yake ilibadilika na
kukosa nguvu na kushindwa kujimudu kwa lolote.
Alisema wakati akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alifariki dunia.
Kaimu Kamanda alisema uchunguzi wa mwili wa marehemu umefanyika
ambapo amekutwa na jeraha kichwani linalovuja damu, alitokwa na damu
puani na masikioni, uvimbe katika jicho la kulia na michubuko midogo
mikononi.
“Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na
uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea,” alisema Kaimu Kamanda.
Alitoa wito kwa mtu au watu wenye taarifa kuhusiana na tukio hili
washirikiane na Jeshi la Polisi kuwafichua watu waliofanya uhalifu huo
ili sheria ichukue mkondo wake.

0 comments:
Post a Comment