ALIYEWAHI
kuwa Naibu Waziri wa Ajira, kazi na maendeleo ya Vijana katika Serikali
ya awamu ya nne,na mbunge wa jimbo la Segerea,Dr Milton Makongoro
Mahanga ameibuka na kuuchambua uteuzi wa Rais Magufuli kwa makatibu na
manaibu wao kwa kudai kuwa hakushauriwa vizuri.
Katika
waraka wake alioundika kupitia ukurasa wake wa Facebook,Dr Makongoro
amesema kuwa kitendo cha Rais Magufuli kuteua makatibu wawili katika
wizara moja hakuja punguza ukubwa wa Serikali yake bali kumeongeza.
Huu hapa waraka huo
MAGUFULI HAKUPUNGUZA UKUBWA WA SERIKALI, AMEONGEZA.
Kwa kuteua makatibu wakuu 2MA7
kiuhalisia rais magufuli kaunda serikali yenye wizara 27 huku
akituaminisha kwamba ni wizara 19. Hivyo siyo kweli kwamba kapunguza
ukubwa wa serikali bali kaongeza ukubwa wa serikali.
Sina
hakika kama wasaidizi wa rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si
ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu (mtendaji mkuu,
afisa masuhuli). Mtendaji mkuu ndiye mwenye dhamana. Ndiyo maana hata
katika ngazi ya kata, ofisi ile inaitwa Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata
siyo ofisi ya Diwani.
Kwa
hiyo magufuli alipounda, kwa mfano, wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi
(ambazo zilikuwa wizara mbili kabla) na kuteua makatibu wakuu (maafisa
masuhuli) watatu kiuhalisia hakuunganisha wizara mbili kuwa moja bali
ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali. Ameongeza ukubwa wa serikali.
Kwa
hiyo anazoita wizara tano za (1) bunge, uratibu, kazi, ajira na
walemavu; (2) kilimo, mifugo, na uvuvi; (3) ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano; (4) viwanda, biashara na uwekezaji; (5) Afya, maendeleo ya
jamii, jinsia, wazee na watoto, na akateua makatibu wakuu 13 kwenye
wizara hizo 5, kiuhalisia ameunda wizara 13 hapo ambazo kabla ya hapo
zilikuwa wizara 11.
Lazima
ieleweke kwamba ukubwa wa serikali hautegemei sana wingi wa mawaziri
bali wingi wa makatibu wakuu. Nitaeleza kwa kutoa mfano wa gharama.
Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha
na kuongeza katibu mkuu mmoja. Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni
mbunge mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki 5
tu juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama zingine ndogo za gari n.k.,
na pia mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva.
Lakini katibu mkuu anaingia upya na mshahara kamili na gharama zingine
nyingi na wasaidizi. Aidha kwa mfano wa wizara ya kilimo, mifugo na
uvuvi kwenye makatibu wakuu watatu lazima kila katibu mkuu atakuwa na
idara na wakurugenzi kadhaa. Kama kwa mfano kitengo cha uvuvi kilikuwa
na idara moja au mbili katibu mkuu mpya wa uvuvi atataka kuongeza idara
na wakurugenzi zaidi. Hizo ni gharama za ziada kwa serikali..
Kumbuka
katibu mkuu awe na naibu au hapana si hoja, hoja ni kwamba atakuwa na
idara kadhaa zenye wakurugenzi (wanaotakiwa kuwa wataalam wa fani za
idara yao). Kwa mfano bila kujali ukubwa wa wizara, kwa mfano, ya
kilimo, ufugaji na uvuvi, rais magufuli angeteua katibu mkuu mmoja (na
naibu wake) halafu akateua wakurugenzi wazuri ambao ni wataalamu kila
mmoja kwenye idara za kilimo, ufugaji na uvuvi. Sasa ukiwa na
wakurugenzi kama hao makatibu wakuu kila kitengo wa nini? Labda rais
magufuli atuambie kwamba hatateua tena wakurugenzi wa kilimo, wa mifugo
na wa uvuvi, na kwamba hao makatibu wakuu wa vitengo hivyo watatosha.
Lakini hili haliwezekani.
Ukiacha
hayo ya msingi sasa angalia hii mpya aliyofanya rais magufuli kwenye
wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji. Ameteua naibu katibu mkuu
mmoja kuwa chini ya makatibu wakuu wawili! Kwa tuliosoma "chain of
command" kwenye "management" tunajua kwamba kila mtumishi lazima awe na
"immediate boss" mmoja tu. Sasa huyu naibu katibu mkuu bosi wake hasa
atakuwa katibu mkuu wa viwanda au katibu mkuu wa biashara na uwekezaji?
Na je mabosi hawa wawili wote wakimpa kazi kwa wakati mmoja ataanza na
kazi ya yupi? Na je yule ambaye kazi yake itacheleweshwa (kwa sababu
naibu katibu mkuu kaanza na kazi ya katibu mkuu mwingine) atajisikiaje
au atachukua hatua gani katika enzi hizi za hapa kazi tu? Au itabidi
makatibu wakuu hawa wawili washauriane kwanza kabla ya kumpa majukumu
naibu katibu mkuu wao?
Kwa
ujumla ahadi ya magufuli kwenye kampeni kwamba ataunda serikali ndogo
hakuitimiza. Ameongeza ukubwa wa serikali. Rais magufuli atambue kwamba
udogo wa baraza la mawaziri kamwe si udogo wa serikali.
Dr. Milton Makongoro Mahanga

0 comments:
Post a Comment