MFANYABIASHARA Morris John ‘Maliyanga’ (46) na wenzake watatu,
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu
shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha wa vitu mbalimbali zikiwemo
dola za Marekani zenye thamani ya sh. milioni 18.5.
Maliyanga, mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam, dereva pikipiki Frano
Msaru au Singu (23) na wafanyabiashara Jeremiah Flavian (26) wakazi wa
Sinza na Sandru Kamugisha (39), mkazi wa Kijitonyama, walifi kishwa
mahakamani hapo jana.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen
Riwa, ambapo Wakili wa Serikali, Honolina Mushi, aliwasomea shitaka
hilo. Akiwasomea shitaka hilo, Honolina alidai washitakiwa walitenda
kosa hilo, Desemba 22, mwaka jana, maeneo ya Mabibo Ruhanga, wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam.
Alidai siku hiyo washitakiwa hao waliiba dola za Marekani 8,600 (sawa
na sh. milioni 18.5), fedha taslim sh. milioni 2.5, kompyuta mpakato,
simu nne za mkononi mali ya Anderson Aloyce.
Inadaiwa kabla na baada ya kutenda kosa hilo, washitakiwa hao
waliwatishia Zeno Genes, Aneth Paulo na John Renatus kwa bastola ili
waweze kufanikisha kupata vitu hivyo. Washitakiwa hao walikana shitaka
hilo, ambapo Wakili Honolina, alidai upelelezi haujakamilika na kuomba
shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Kwa upande wa mshitakiwa Msaru aliomba apewe kibali cha kwenda
kutibiwa mguu kutokana na majeraha aliyodai kuyapata baada ya kupigwa
akiwa polisi.
Hakimu alimtaarifu mshitakiwa huyo kwamba atapata matibabu kwa kuwa
Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kutoa huduma hiyo. Pia, aliahirisha
shauri hilo hadi Januari 27, mwaka huu kwa kutajwa na kusema washitakiwa
watarudishwa rumande kutokana na shitaka linalowakabili kutokuwa na
dhamana kwa mujibu wa sheria.

0 comments:
Post a Comment