Zaidi
ya wakazi laki tatu kutoka kata zote 36 zilizoko halmashauri wilaya ya
Chamwino mkoani Dodoma wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa
muda mrefu ambapo hivi sasa wanalazimika kula wadudu jamii ya viwavi
matunda ya porini, mizizi na uji wa ubuyu ili kujinusuru na vifo huku
pia kukiwa na taarifa za watu watatu kupoteza maisha mmoja kati yao
akijinyonga kwa sababu ya njaa.
Ni katika eneo la kata ya chamwino ikulu jirani na ikulu ndogo ya
rais iliyopo wilayani hapa ambapo mama huyu na wakazi wengine kutoka
maeneo mbalimbali wanalazimika kuja kushinda sehemu hii ili kujipatia
angalau mlo ambao ni matunda aina ya zambarau ,
baadhi yao ambao wanadai tatizo la njaa ni kubwa wilayani humo hali
inayochangia shughuli zingine ikiwemo za kilimo kusimama huku pia baadhi
ya wazazi wakizikimbia familia.
Kufuatia tatizo hilo inawalazimu wajumbe wa baraza la madiwani wa
jimbo la Chilonwa wilayani Chamwino kukutana ambapo viongozi hao
wanashusha lawama kwa maofisa wa idara ya maafa chini ya ofisi ya waziri
mkuu kuwa wameshindwa kuwasaidia wananchi licha ya kupokea taarifa mara
kwa mara huku wakiishia kufanya tathmini na kutoa tani 150 tu za
mahindi ambayo hata hiyo hayakidhi mahitaji.
Katika kuonyesha uhalisia wa tatizo la njaa Mussa Omari diwani wa
kata ya majereko anaingia katika kikao hicho na mkebe wenye wadudu jamii
ya viwavi jeshi ambao anadai yeye na wananchi wake walilazimika kuamka
saa tisa usiku na kwenda porini kuwatafuta kwa ajli ya mlo.
Kwa upande wake afisa kilimo wa wilaya ya Chamwino Geofrey Nyamale
anakiri kuwa baa la njaa ni kubwa wilayani humo kwani hali hiyo ilianza
kujitokeza tangu mwezi may mwaka jana ambapo ofisi yake imekuwa ikifanya
jitihada kubwa za kuomba chakula cha msaada lakini hawapati majibu
sahihi kutoka ngazi za juu huku akibainisha kuwa msaada wa chakula
unaohitajika hizi sasa ni zaidi ya tani 14000.
0 comments:
Post a Comment