WAKAZI wa Mtaa wa Lingato eneo la Kigamboni, katika Manispaa ya
Temeke jijini Dar es Salaam na wengine kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji,
wamevamia eneo la ekari 3,000 na kujikatia maeneo baada ya eneo hilo,
lililokuwa la mwekezaji kurudishwa kwa wanakijiji.
Kutokana na hilo, baadhi yao wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati kuzuia uvamizi huo,
ambao maofisa wa Ardhi wamethibitisha kuwa wanaofanya hivyo ni wavunjifu
wa sheria.
Kaimu Kamishna wa Ardhi ambaye hakutaka kutaja jina, alipozungumza na
gazeti hili jana, alisema mambo hayo yanayoendelea hayana kibali
kisheria na kwamba uvamizi ni kinyume cha sheria na watachukuliwa hatua.
“Hatuna taarifa hiyo rasmi, lakini kuna mwananchi alipiga simu
akasema kuna watu wamevamia ardhi na kugawana… hiyo ni Kisarawe II iko
chini ya Manispaa ya Temeke, wao hawana mamlaka ya kufanya wanayofanya,”
alisema Kaimu Kamishna huyo.
Kwa mujibu wa wanakijiji wa Lingato na waliotoka maeneo mengine,
walidai walifika hapo kwa lengo la kupata ardhi bure baada ya kuelezwa
kuwa kijiji hicho kinagawa ardhi hiyo kwa wananchi. Hata hivyo,
walilalamikia ugawaji huo kuwa umejaa urasimu.
Katika eneo hilo walikutwa wananchi kutoka sehemu mbalimbali jijini,
wakijikatia maeneo na kuweka alama zao huku wakiwa wanalinda maeneo yao
wakidai kutotaka urasimu unaoendelea. Baada ya gazeti hili kupata
malalamiko hayo na kwenda katika eneo hilo, lilikuta kundi kubwa la watu
ambao walikuwa wakielekea huko kujipatia ardhi kama walivyoelezwa,
lakini walilalamikia kuwapo na ubabaishaji.
“Hapa tunamtaka aje Waziri wa Ardhi asimamie au atoe mwongozo wa
zoezi hili, kumekuwa na urasimu mkubwa watu wanazungushwa bila kupata
taarifa sahihi na viongozi hawajulikani ni kina nani,” alisema Athumani
Mponda.
Wananchi hao walidai kuna baadhi ya watu wanaojiita wajumbe wa kamati
ya ugawaji viwanja hivyo, wamekuwa wakidai fedha kwa watu wanaofika
kupata viwanja ingawa walielezwa kuwa viwanja vinatolewa bure.

0 comments:
Post a Comment