TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Katavi
inamshikilia Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kawajense, Manispaa ya Mpanda
Catherine Kipeta kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh 30,000.
Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Katavi, Christopher Nakua alisema
kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 18, mwaka huu katika eneo la Mtaa
wa Kawajense baada ya kuandaliwa mtego ambao ulifanikisha kukamatwa
kwake.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Ofisi ya Takukuru kupokea
taarifa kutoka kwa mlalamikaji kuwa Ofisa Mtendaji huyo anamuomba rushwa
kiasi cha Sh 30,000 ili asimpeleke kwenye Baraza la Kata kwa kosa la
kufungua sehemu yake ya biashara wakati ni muda wa kufanya usafi na
kutokushiriki kufanya usafi.
Ilidaiwa kuwa baada ya kupokea taarifa hizo ofisi ya Takukuru
ilifanya uchunguzi na baada ya kuridhika na maneno ya mlalamikaji ndipo
mtego ulipoandaliwa na mtuhumiwa kukamatwa.
Kamanda Nakua alisema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa
mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili ambazo ni kuomba rushwa ya fedha
taslimu Sh 30,000, shtaka la pili litakuwa ni kupokea rushwa ya Sh
30,000 kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria ya kuzuia na
kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007.

0 comments:
Post a Comment