Tuesday, January 26, 2016




HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara imekataa kupokea hundi ya takribani Sh bilioni 1.060 za malipo ya tozo ya huduma zilizotolewa na kampuni ya Acacia ya uchimbaji wa madini katika Mgodi wa North Mara wilayani hapa.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Moses Yomami akitangaza uamuzi huo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, alisema wamegoma kupokea malipo hayo kutokana na kukosekana taarifa sahihi ya kiasi halisi cha dhahabu inayozalishwa katika mgodi huo.

Awali kabla ya Meneja wa mgodi huo, Garry Chapman kukabidhi hundi hiyo, mwenyekiti huyo alimkatiza akisema kumekuwepo mapungufu makubwa katika uwasilishaji wa fedha katika halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na mrabaha na tozo ya ushuru katika siku za nyuma na kuzusha maswali kutoka kwa madiwani juu ya uwazi wa kiasi halisi cha dhahabu kinachopatikana baada ya uchimbaji.

Pia mwenyekiti huyo alieleza changamoto inayokabili halmashauri ya kupata hasara wakati wa kuhamisha fedha hizo kuelekea katika akaunti ya umma kutokana na malipo hayo kufanywa kwa dola za Kimarekani na kupata hasara isiyo ya lazima kutokana na viwango vya ubadilishanaji kubadilika kila mara.
 
Pia katika hatua nyingine alitaka kampuni hiyo iwasilishe orodha ya kampuni tanzu zinazohudumu katika mgodi huo ili waweze kufanya tathmini juu ya mchakato wa kampuni hizo pia kulipa ushuru wa huduma kama sheria inavyoagiza ili kuongeza kipato cha halmashauri.

0 comments:

Post a Comment