SERIKALI imetangaza utaratibu mpya wa utekelezaji wa mpango wake wa
kubomoa nyumba zote zilizojengwa kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Imesema hivi sasa itajielekeza kubomoa nyumba zilizo ndani kabisa ya
bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na katika kingo za Bonde la
Msimbazi.
Sambamba na hilo, imesema itaheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya
mashauri ya watu walioweka pingamizi la nyumba zao kubomolewa na
itawalipa fidia wale wote waliojenga kwenye maeneo hatarishi kwa kupewa
vibali halali na Serikali na pia itafuatilia kesi zilizoko mahakamani
ili ziishe haraka tayari kwa taratibu nyingine kuendelea.
Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, January Makamba, mbele ya waandishi wa habari wakati
akitoa taarifa ya mkutano wa mawaziri watatu walioketi kufanya tathmini
ya mwenendo wa kazi hiyo na kuibuka na maazimio 12 yanayoelekeza namna
mpya wa utekelezaji wa ubomoaji.
Mawaziri waliofikia pamoja na Makamba kufanya tathmini hiyo ni Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Injinia Ramol Makani.
Aidha, tangazo la uamuzi huo mpya wa Serikali limekuja ikiwa ni siku
chache baada ya Rais John Magufuli kukutana kwa nyakati tofauti na
marais wawili wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete pamoja na
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Makamba alisema kazi ya
kuwaondoa wananchi wanaoishi katika Bonde la Msimbazi itaendelea kwa
utaratibu ambao hautawasababishia mateso na usumbufu.
Alisema utekelezaji wa kazi ya ubomoaji ndani ya bonde hilo utalenga
makazi yote yaliyojengwa ndani kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya
kuingia bondeni na katika kingo za bonde.
Waziri Makamba alisema watu wenye nyaraka halali zilizowaruhusu
kujenga walizopewa na mamlaka za umma hawatahamishwa bila kupewa sehemu
nyingine za kujenga na kwamba watumishi wa umma waliotoa maeneo hayo
watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
Akizungumzia maeneo yaliyokwishabomolewa alisema katika muda wa siku
tatu kuanzia jana, kazi ya kuzoa vifusi na kusafisha maeneo
yaliyobomolewa itaanza.
Akizungumzia ukiukwaji wa taratibu dhidi ya baadhi ya maofisa wa
Serikali, Waziri Makamba alisema Serikali itawachukulia hatua za
kinidhamu watumishi wake wanaoendesha kazi ya kubomoa na kuweka alama ya
X katika nyumba zinazopaswa kubomolewa kinyume na misingi ya sheria
zinazotekelezwa.
“Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake ambao
watakwenda kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwamo wanaoweka alama
za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria, limeanzishwa dawati la
malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu kazi hii.
“Pia nyumba na majengo yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa
sheria zinazotekelezwa sasa hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya
watu yalipo hatarini,” alisema Makamba.

0 comments:
Post a Comment