MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana wilayani Mpwapwa, imesababisha kaya 30 katika kijiji cha Gulwe kukosa makazi.
Aidha mvua zimeharibu ekari 47 za mashamba ya mazao mbalimbali.
Diwani wa Kata ya Gulwe, Gabriel Kizige alisema pamoja na maafa hayo pia
maji yameingia katika nyumba 50 na kusababisha mali kuharibika ikiwemo
chakula.
Akitoa taarifa ya madhara yaliyopatikana mbele ya Kamati ya Maafa,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Gulwe, Peter Sogodi alisema kuwa nyumba 30 za
wakazi wa hapo zilibomoka, nyumba 50 ziliingia maji na ekari 47 za mazao
mbalimbali ziliharibika kwa kusombwa na maji.
Aidha Ofisa Mkaguzi wa njia ya treni Stesheni Gulwe, Moses Magoha
alisema pia mvua hiyo imesababisha njia ya reli hiyo kufukiwa kwa
mchanga na zaidi mita 26 za reli imebomolewa na mvua hiyo.
Akizungumza mmoja wa wananchi, Elizabeth Stephen alisema mvua hiyo
ilinza kunyesha majira ya saa 9:00 usiku na kusababisha maafa hayo
katika kijiji chao.
Hata hivyo imeelezwa kuwa baadhi ya kaya zilizokumbwa na mafuriko ni
zile ambazo awali zilihamishwa kupelekwa maeneo salama na kurejea katika
makazi yao ya zamani ambayo ni mkondo wa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Utaly amewataka waathirika wa
mafuriko hayo kutokurudi tena katika makazi hayo ya zamani ambayo ni
hatarishi kwa maisha yao.
Aidha alisema katika hatua za awali wananchi hao wataweza kusaidiana
na serikali itakayotoa sehemu ya chakula cha njaa kuweza kusaidia kaya
zilizoathirika na mafuriko kwa sehemu kubwa.

0 comments:
Post a Comment