Saturday, January 2, 2016




Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo ,Anna Mughwira amewahimiza waandishi wa habari mkoani hapa, kutumia taaluma yao kuwaelimisha wazazi/walezi juu ya madhara watakayopata wanafunzi watoro, ili waweze kutoa ushirikiano wa kukomesha vitendo hivyo.

Mwenyekiti huyo ametoa wito huo wakati akishiriki ajenda ya utoro na mimba kwa wanafunzi kwenye kikao cha kamati ya ushauri (RCC) mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.

Alisema vitendo vya utoro na mimba kwa wanafunzi havivumiliki, kwa madai vinasababisha wahusika kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.

“Kama mnavyojua kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha, elimu bora inamsaidia mhusika kumudu maisha yake. Mwanafunzi awe mtoro wa reja reja au utoro wa kudumu,anajikosesha haki yake ya msingi na kwa vyo vyote maisha yake yatakuwa mabaya”,alisema.

Kwa hali hiyo,mwenyekiti huyo amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kukomesha vitendo vya utoro mashuleni.

“Waandishi wa habari mliopo hapa, tumieni vizuri taaluma yenu kuwaelimisha na kuwahamasisha wazazi kusimamia watoto wao kuhudhuria shuleni bila kukosa,ili kuboresha taaluma na mwisho wa siku, wafanye vizuri kwenye mitihani yao”, alifafanua Mughwira.

0 comments:

Post a Comment