
Polisi
na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanachunguza mzigo
ulioingizwa nchini na kampuni ya StarTimes na kuhifadhiwa kwenye ofisi
zake zilizo ndani ya uzio wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC),
Mikocheni, Dar es Salaam.
Polisi
pia inachunguza kama bidhaa zinazoingizwa na kampuni hiyo ni zile
zinazotumika kwenye biashara ya ving’amuzi au kwa ajili ya shughuli
nyingine, kwa mujibu wa ofisa mawasiliano wa TRA.
StarTimes
ni kampuni ya China inayofanya biashara ya kuuza ving’amuzi kwa ajili
ya vituo mbalimbali vya televisheni, hasa vya TBC.
Habari
ambazo gazeti hili imezipata kutoka vyanzo mbalimbali, zinaeleza kuwa
mzigo huo unaosadikiwa pia kuwa na simu za mkononi na vifaa vya
pikipiki, uliingizwa juzi na kuhifadhiwa kwenye ofisi za StarTimes.
Habari
hizo zinasema kuwa baada ya TRA kuutilia shaka mzigo huo, ilituma
maofisa wake ambao walikesha usiku wa kuamkia jana kuufanyia upekuzi ili
kujua kama unalingana na bidhaa zilizoko kwenye nyaraka walizotumia
kuuingiza nchini.
Gazeti
hili lilifika ofisi za kampuni hiyo jana saa 3.30 asubuhi kupata
ufafanuzi juu ya taarifa hizo, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuzungumza
lolote, kwa madai kuwa mmoja wa waandishi hao wa habari alipiga picha
jengo la kampuni hiyo bila ya ruhusa.
Mmoja
wa walinzi wa kampuni hiyo, alikanusha taarifa za kukamatwa kwa mizigo
ya kampuni hiyo, akisema “hakuna kontena wala mzigo ulioingizwa hapa, na
kama kontena zingekuwepo si mngeziona”.
Juhudi
za kuzungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya StarTimes, Clement Mshana
ziligonga mwamba baada ya askari aliyejitambulisha kwa jina la Isack
Mwakyembe kusema ameagizwa na viongozi wa juu kutoruhusu mwandishi wa
habari kutoka chombo chochote zaidi ya TBC kuingia.
“Nimepewa maagizo asubuhi ya leo kwamba humu ndani asiingie mwandishi na mimi nafuata utaratibu huo,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA,
Richard Kayombo alisema kulikuwa na utata katika upangaji wa mizigo wa
simu za mkononi zilizoletwa na Startimes.
“Watu
wetu wako hapo StarTimes kuhakiki na kujiridhisha juu ya taarifa hizo.
Tutawajulisha baadaye.” Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro alisema apigiwe simu baada ya saa mbili kwa kuwa
alikuwa kwenye kikao. Hata hivyo, alipotafutwa baadaye, hakupatikana.
0 comments:
Post a Comment