GAZETI la Marekani la Sun Times na lenye umaarufu barani Afrika, limemtangaza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kama rais bora wa mwaka 2015 kwa Afrika.
Gazeti hilo pia limewataja watu wengine bora wa mwaka na kampuni bora yenye mchango kwa jamii.
Makundi ya tuzo yaliyokuwepo ni pamoja na mtu bora wa kimataifa wa mwaka, kiongozi bora wa Afrika, kampuni yenye mchango bora kwa jamii ya mwaka, mwanamajumuhi wa Afrika wa mwaka, mtu bora anayeishi uhamishoni, mtu mwenye ushawishi mwenye umri chini ya miaka 40 na balozi bora wa utalii kwa Afrika.
Katika makundi hayo, Rais Kikwete aliyeitawala Tanzania tangu mwaka 2005 hadi 2015, ametajwa kuwa kiongozi bora wa Afrika wa mwaka 2015.
“Rais Kikwete ameitumikia nchi yake kwa miaka 10 ya mihula miwili na ameshiriki moja kwa moja katika uteuzi wa mrithi wake, Rais John Magufuli hivyo kuendeleza utamaduni wa kidemokrasia wa kubadilishana madaraka, tofauti na nchi jirani na Tanzania ambazo viongozi wake wamekuwa wakivunja Katiba ili kuendeleza matamanio yao ya kisiasa,” limesema gazeti hilo.
“Rais Kikwete amepokea heshima nyingi kwa utendaji wake bora na shahada za udaktari wa heshima kutoka vyuo vikuu vingi. Afrika itaendelea kumhitaji kwa upatanishi wa amani alioufanya si alipokuwa tu rais, bali hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10.”
The African Sun Times ni gazeti kubwa zaidi la wiki nchini Marekani na limekuwa likichapishwa kwa miaka 37 iliyopita.
Mhariri wake mkuu Dk. Chika Onyeani ameshinda tuzo 73 za uzoefu katika uandishi wa habari na kujihusisha na utetezi wa haki za binadamu.
Dk. Onyeani pia ni mwandishi wa vitabu maarufu kama vile Capitalist Nigger: The Road to Success, Roar of the African Lion, The Broederbond Conspiracy (The Black James Bond) na kitabu cha watoto “ODUM: The Lion.”
Mbali na Rais Kikwete, tuzo ya mtu bora wa kimataifa wa mwaka 2015 imekwenda kwa Rais wa zamani wa Serikali ya Shirikisho la Nigeria, Goodluck Jonathan.
“Jonathan aliushtua ulimwengu baada ya kumwita Rais wa sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari na kukubali kushindwa uchaguzi wa Machi 29, 2015 na hivyo kusitisha hofu ya kutokea vurugu na umwagaji wa damu katika nchi hiyo huku akiahidi kutoruhusu damu za Wanaigeria kutumika katika matamanio yake kisiasa,” limeandika gazeti hilo.

0 comments:
Post a Comment