Friday, January 29, 2016

HOTUBA ya Rais Dk. John Magufuli, imeendelea kujadaliwa bungeni, huku baadhi ya wabunge wakionekana kufurahishwa na kasi ya utendaji wa kiongozi huyo katika kipindi kifupi alichokaa Ikulu.
Akichangia hoja hiyo bungeni jana, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliishauri Serikali kuwasilisha bungeni sheria zote zinazokinzana na kasi ya Dk. Magufuli ili ziweze kufanyiwa marekebisho.Bashe alisema yapo malalamiko mbalimbali kuwa kasi ya rais inayofanyika hivi sasa imekuwa ikikinzana na baadhi ya sheria za nchi.Mbunge huyo alisema baadhi ya sheria zilizopo hivi sasa zimekuwa ni kichaka kikubwa cha wezi wanaoliibia taifa.
Akitoa mifano, aliitaja Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004 kuwa ni kati ya sheria zinazohitaji kurekebishwa, kwani imekuwa ikitoa mwanya kwa watumishi wa Serikali kuliibia taifa.
“Utaona kwa kutumia sheria hiyo, tundu la choo linajengwa kwa Sh milioni 20, kupitia wakandarasi wao, wakati choo hicho hata milioni tano hazifiki,’’ alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kunahitajika kiongozi kama Dk. Magufuli katika kufanya uamuzi sahihi ili jamii iweze kuondoka hapa ilipo na kupiga hatua.
“Watu wanahoji eti kwanini Serikali imetoa fedha na kupeleka shuleni bila kupitia bajeti ndogo, sasa ulitaka watoto wetu wasiende shule,’’ alisema.
Bashe alisema hotuba hiyo ya rais aliyoitoa bungeni imetoa taswira kuwa Dk. Magufuli ndiye rais ambaye Watanzania walikuwa wakimhitaji kwa ajili ya mageuzi nchini.
Aidha mbunge huyo aliiomba Wizara ya Fedha kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa reli kwa ukubwa wa ‘standard gauge’.
Alisema reli ni njia muhimu ya kusafirisha mizigo mbalimbali ikiwamo hata ya nje ya nchi.
“Tumeona ‘political will’ (utashi wa kisiasa) ya rais kuifanya nchi kuwa ya viwanda, lakini yako mengi tunapaswa kuyafanya kama wabunge.

- See more at: http://edwinmoshi.blogspot.com/2016/01/bashe-alia-na-sheria-zinazokinzana-na.html#sthash.xXuszNmx.xsr4Bt27.dpuf

0 comments:

Post a Comment