Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi
Meck Sadiki amewataka waliovamia na kujigawia maeneo ya watu wengine
likiwamo la Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na aliyewahi kuwa
Naibu Waziri wa Ardhi, Ritha Mlaki waondoke mara moja kwa kuwa wamevunja
sheria.
Alisema zaidi ya watu 2,000 wakiwamo waliobomolewa nyumba katika baadhi
ya maeneo jijini Dar es Salaam wamevamia na kujigawia mashamba hayo
yaliyopo Tegeta na Goba kinyume cha sheria.
“Kisa wamevunjiwa nyumba zao walizojenga kinyume cha sheria ndiyo
wameamua kuvamia maeneo yasiyo yao, hili ni kosa kama makosa mengine,
nawataka waondoke haraka vinginevyo tutawachukulia hatua kali za
kisheria,” alisema mkuu huyo wa mkoa. Alisisitiza kuwa agizo la Rais John Magufuli lilikuwa ni maeneo
yaliyoachwa wazi kuainishwa kwa ajili ya kupangiwa matumizi mengine na
siyo kuruhusu watu kuvamia bila taratibu.
Hakuna viwanja
Sadiki alisema hakuna viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya kuwagawia
wananchi waliokumbwa na bomoabomoa katika maeneo ya mabondeni.
Zaidi ya nyumba 8,000 zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, fukwe
za bahari na kando ya mito zimeanza kubomolewa kabla ya kusitishwa na
Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sadiki alisema wananchi
waliobomolewa nyumba zao na ambao watakumbwa na operesheni hiyo
wasitarajie kupatiwa viwanja vya kujenga nyumba zao.
Bomoabomoa hiyo inaendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ikiwalenga waliojenga kinyume cha sheria.
“Serikali haina viwanja vinavyotosha kuzigawia familia zaidi ya 8,000
zitakazobomolewa, niwashauri tu wasiendelee kupoteza muda wao kwa
kuwasikiliza wanasiasa, watafute makazi mengine waende. Kama
walivyovamia na kujenga ndivyo wanatakiwa kutafuta maeneo mengine
wahamie,” alisema Sadick.
Alisema viwanja 1,007 vya Mabwepande vilitolewa kwa wananchi waliokumbwa
na mafuriko mwaka 2011 ambao waliwekwa kwenye kambi baada ya kukosa
makazi.
Alisema kaya zote zilizokosa makazi kutokana na mafuriko hayo zilipatiwa
maeneo. Waathirika 580 walitokea Ilala, Kinondoni 349 na Temeke 81.
“Kuna upotoshaji unaendelea kwamba yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
kuwapatia wanaobomolewa sasa, jambo hili halina ukweli, ikumbukwe
tuligawa viwanja vya Mabwepande baada ya Rais (Jakaya Kikwete) kuagiza
tufanye hivyo ili kuwasaidia wale tu, waliokumbwa na mafuriko,” alisema.
Sadiki alisema kinachoendelea kwenye eneo la Mabwepande ni uandaaji wa hati za viwanja na tayari kaya 102 zimeshapatiwa.
Alisema Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) iliikopesha Manispaa ya
Kinondoni zaidi ya Sh17.5 bilioni kwa ajili ya kupima viwanja katika
eneo hilo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment