BUNGE limetoa idhini kwa mawaziri walioteuliwa na Rais John Magufuli
ambao hawajala kiapo cha ubunge kushiriki shughuli za kibunge.
Limesema wateule wa Rais Magufuli katika nafasi za uwaziri ambao
kwanza waliteuliwa kuwa wabunge watakula kiapo cha ubunge wakati wa
mkutano wa pili wa Bunge la 11, ili kutimiza matakwa ya kikatiba na
kanuni za Bunge kabla ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yao ndani ya
Bunge.
Msimamo huo wa Bunge umetolewa jana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashilillah, wakati wa mahojiano na gazeti hili kupitia simu yake ya
kiganjani kuhusu uhalali wa mawaziri hao kushiriki shughuli za kibunge
kabla ya kuapishwa.
Dk. Kashilillah alisema Katiba na Kanuni za Bunge hazimzuii Rais
kuteua wabunge na kuwapa nafasi za uwaziri, wakati ambao Bunge
halikutani na badala yake amepewa mamlaka ya kikatiba katika Ibara ya 55
ya kuteua mtu kuwa waziri na Ibara ya 56 inampa mamlaka ya kumwapisha.
Alisema kwa muktadha huo, Katiba na Kanuni za Bunge haziweki mipaka ya wakati wabunge kuchaguliwa au kuteuliwa.
“Rais hafungwi na masharti yaliyo kwenye ibara ya 68 ya Katiba kuhusu
kuwaapisha wabunge kabla ya kuanza kushiriki shughuli za Bunge kwa
sababu tafasili ya shughuli za Bunge imewekwa wazi na Ibara ya 63 ambayo
kimsingi inasema ni shughuli za Bunge ndani ya Bunge na kamati zake.
“Hivi sasa Kamati za Bunge bado hazijaundwa na Spika mpaka mkutano wa
pili wa Bunge la 11 utakapoanza Januari 26, mwaka huu. Lakini hata kama
itatokea kamati inafanya kazi zake kabla ya Bunge kukutana, kama kuna
waziri ambaye hajaapishwa kuwa mbunge, rais ana mamlaka ya kumkaimisha
waziri mwingine ambaye amekwishaapishwa kuwa mbunge kushikiri shughuli
hizo.
“Leo nimeongea na waandishi wa habari wengi sana walionipigia simu
wakiulizia hili kwa sababu naona limekuwa na mjadala mkubwa. Haya mambo
ya kibunge ni vizuri kuyaelewa kwanza kwa sababu hata
Kanuni za Bunge
zimetoa nguvu kwa kamati kujipangia utaratibu wake wa kazi na kuwaruhusu
watu ambao si wabunge au wabunge ambao si wa wajumbe wa kamati husika
kushiriki katika vikao,” alisema Dk. Kashilillah.
Alisema kwa ruhusa hiyo iliyotolewa na Kanuni ya 117 (8), mawaziri
walioteuliwa na Rais Magufuli wanaweza kushiriki kwenye shughuli za
Kamati za Bunge pasipo kuhesabiwa kuwa ni wajumbe rasmi.

0 comments:
Post a Comment