Rais John Magufuli.
Viongozi wa madhehemu ya dini mbalimbali nchini wanakutana leo jijini Mwanza kwa ajili ya kufanya maombi maalum ya kumtakia afya njema na maisha marefu Rais John Magufuli.
Maombi hayo yatafanyika katika viwanja vya Furahisha jijini hapa na kuhudhuriwa na wananchi, waumini wa dini zote, viongozi wa dini pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo.
Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa Kanisa la Good News for All Ministries, ambao wanaratibu shughuli za maombi hayo, Mchungaji Palemo Masawe, alisema dini zote zimekaribishwa kushiriki maombi hayo. Alisema maombi hayo ni kwa ajili ya watu wote bila kujali dini zao kumuombea afya njema na maisha marefu Rais Magufuli ili aweze kuwatumikia wananchi ipasavyo na bila ya vikwazo kutoka kwa watu wasiomtakia mema na taifa kwa ujumla. Mchungaji huyo alisema baada ya kumaliza maombi hayo, watafanya maombi mengine ya kuombea ukomeshaji wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema mauaji mengine watakayoombea yakomeshwe na Mungu ni ya wazee na vikongwe katika mikoa hiyo. “Ni laana kuwapo kwa mauaji ya namna hii, hivyo kupitia maombi haya tutamuomba Mungu ayakomeshe kabisa na kuyatokomeza,” alisema.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Good News for All Ministries, Charles Gadi, alisema maombi hayo yatakuwa ya aina yake kwa kuwa viongozi wengi wa dini zote watashiriki.
“Unajua Magufuli anafanya kazi nzito na ngumu na mara nyingi amewaomba Watanzania kumuombea kwa Mungu na sisi tumeguswa kufanya hivyo kwa kushirikiana na wananchi wote,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment