BARAZA
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanza kung’ata
kwa kutumia kanuni ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kelele na
mitetemo.
Kwa
sasa mtu akitaka kufanya sherehe mtaani, kupiga muziki kwa kelele,
kuendesha ngoma za kukesha za nusu uchi (vigodoro) au ‘bai koko’ au
kufanya ibada kwa kelele mitaani, atapaswa kulipa Sh milioni 10.
Pia, baa na kumbi za starehe za usiku zitakazopiga kelele, zitapaswa kulipa kiasi hicho.
Aidha,
NEMC imesema pia kuwa wale watakaohusika na kelele za migodini za
kutumia baruti, kupasua miamba zilizo zaidi ya matakwa ya sheria ya
mazingira ya kelele na mitetemo, watapaswa kulipa Sh milioni tano ili
kupata kibali.
NEMC
imetaka watu kuheshimu kanuni za viwango vya kelele na mitetemo katika
maeneo mbalimbali nchini. Imeonya kuwa watakaokiuka, hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao. Kanuni hizo zimeanza kutumika mwaka jana
(2015).
Mkurugenzi
Mtendaji wa NEMC, Bonaventure Baya alisema hayo Dar es Salaam jana.
Alisisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na
mitetemo, umekuwa ukifanyika bila kujali sheria za nchi na sasa
watashughulikia suala hilo ipasavyo.
Alisema
hivi sasa kanuni za kudhibiti suala hilo, zimekamilika na zimeanza
kutumika kikamilifu. Mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha kanuni na
sheria, atachukuliwa hatua kali. Baya alitoa ufafanuzi kuwa yapo maeneo
yenye kelele zaidi ya viwango vinavyoruhusiwa kisheria, ikiwamo maeneo
ya migodini.
Alieleza
kwamba kanuni zimeweka vigezo na tozo maalumu la kuanzia Sh milioni
tano hadi Sh milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo.
Alisema mambo mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni
itakayovunjwa na kusisitiza kuwa hatua hizo zitachukuliwa ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment