WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), George Simbachawene amesema atahakikisha shule zote hapa
nchini zinakuwa na madawati yanayofanana.
Alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari
kuzungumzia changamoto za elimu bila malipo iliyoanza kutolewa Januari
mwaka huu.
“Katika historia ninayotaka kuandika ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi
anayekaa chini katika kipindi cha miaka miwili lazima tuondokane na
tatizo hili,” alisema na kuongeza kuwa atakuja na ubunifu utakaoondoka
tatizo hilo nchini.
“Nataka kuwe na madawati yanayofanana nchi nzima yenye lebo ya For
Government Primary School, ninaona mwanga mkubwa mbele yangu na katika
hili ninaweza kufanikiwa nipeni fursa,” alisema.
Alisema pia kumekuwa na changamoto kubwa ya matumizi ya fedha
zilizopelekwa kwa ajili ya kugharamia elimu na kuongeza lengo la
serikali kutoa elimu bila malipo litabaki pale pale kwani miaka ya nyuma
watoto wengi walishindwa kupata elimu kutokana na gharama kuwa kikwazo
kwao.
Simbachawene alisema changamoto kubwa ni kwa walimu kudhani fedha
zilizopelekwa shuleni ni za mwaka mzima lakini ukweli ni kuwa fedha ni
za kila mwezi.
Alisema kila mwanafunzi wa shule ya msingi ya serikali atatoa
shilingi 10,000 na kwa sekondari ni shilingi 25,000 kwa mwaka kwa ajili
ya uendeshaji wa shule.
Waziri huyo alisema kwa shule za sekondari za kutwa kila mwanafunzi
atapata shilingi 3,540 na kwa shule ya sekondari ya bweni ni shilingi
7,243.
“Ukiwa na wanafunzi 500 maana yake shule inapata zaidi ya shilingi
milioni 3.6 kwa mwezi mmoja tu je ukipata fedha hizo unashindwa
kuendesha shule?” alisema na kuongeza kuwa serikali pia ilipeleka fedha
za chakula ili watoto waweze kula lakini fedha hizo zisitumike kulipa
madeni ya samani ya wazabuni.
Aliwataka walimu wasivunje moyo juhudi zinazofanywa na serikali kwani mzazi masikini amepokea mzigo mzito sana na serikali.
“Tutakapokuja kwenye bajeti ya kwanza ya awamu ya tano tutakuwa
tumejifunza changamoto. Tutaboresha na mambo mengine mazuri yatakuja,”
alisema.

0 comments:
Post a Comment