NEEMA ya gesi ambayo imekuwa ikizungumzwa, inatarajiwa kubadili Mkoa
wa Lindi, kupitia uwekezaji mkubwa ambao haujawahi kutokea katika
historia wa miradi nchini, wenye thamani ya inayofikia zaidi ya dola za
Marekani bilioni 60 na kutoa ajira karibu 20,000.
Taarifa za wadau wa miradi hiyo, ikiwemo Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), zilizowasilishwa kwa wawakilishi wa wananchi
mkoani Lindi wiki hii, zimebainisha kuwa miradi hiyo inahusu ujenzi wa
Mradi wa Kusindika Gesi (LNG) na Kiwanda cha Mbolea.
Kwa mujibu wa taarifa za TPDC, tayari ardhi imepatikana hekta 2,071
kwa ajili ya mradi wa LNG, huku hekta zingine 20,000 zinazozunguka eneo
la mradi huo, zikitengwa kwa ajili ya viwanda.
Kwa sasa kwa mujibu wa taarifa hiyo, TPDC imeshatwaa ardhi hiyo na
kazi inayofanyika ni kufanya uthamini wa mali za wananchi wachache walio
katika eneo hilo, kulipa fidia na kuwahamisha.
Mradi LNG
Akizungumza na wawakilishi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James
Mataragio, amesema kwa kuwa gesi iliyogundulika baharini inayofikia
kiasi cha futi za ujazo trilioni 47, ni nyingi na ikivunwa mahitaji ya
ndani hayawezi kuimaliza, watalazimika kuiuza nje ya nchi na kuongezea
Taifa mapato.
Kutokana na umuhimu huo wa kuuza gesi nje, Dk Mataragio alisema
kitaalamu rasilimali hiyo inapaswa kutolewa kwenye visima na kufikishwa
katika mtambo huo wa LNG, ambao utaigeuza kuwa kimiminika, ili ifae
kuingizwa katika matangi na kusafirishwa kwa meli kwenda katika masoko
mbalimbali duniani.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Kelvin Komba alisema
mtambo huo utaipooza gesi itakayovunwa mpaka nyuzi joto sifuri na
kuipooza zaidi mpaka nyuzi joto hasi 100, ndipo inakuwa kimiminika na
kufaa kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali duniani.
Uwekezaji wenyewe
Taarifa za makampuni yanayoshirikiana katika ujenzi wa mtambo huo
ambayo ni TPDC, BG Group, Ophir Energy, Statoil, ExxonMobil na Pavilion
Energy, zimeeleza kuwa thamani ya mradi huo ni kuanzia dola za Marekani
bilioni 30 mpaka dola bilioni 60.
Akifafanua ukubwa wa uwekezaji wenyewe, Makamu wa Rais wa BG Group
Tanzania, Sera, John Ulanga kwa niaba ya wawekezaji hao, amesema Bajeti
ya Serikali ya Tanzania ni kama dola za Marekani bilioni 10 mpaka 15,
kwa hiyo uwekezaji huo ni sawa na kukusanya mapato ya Serikali kwa miaka
minne, yasitumike popote, isipokuwa Lindi.
Ajira Mbali na ukubwa wa mradi kwa maana ya kiwango cha fedha
kitakachowekezwa, Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Komba alisema wakati wa
ujenzi wa mradi huo utakaochukua miaka minne mpaka saba, kutatolewa
ajira za moja kwa moja zinazokadiriwa kufikia 15,000.
Baada ya ujenzi, wakati wa uendeshaji wa mradi huo kwa mujibu wa Komba, ajira katika mradi huo zitakazotolewa ni za watu 5,000.
Mbali na ajira, Komba ametaja fursa zingine zitakazotokana na
uwekezaji huo unaotarajiwa kuanza wakati wowote, kwamba ni huduma kwa
wafanyakazi hao ikiwemo usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Nyingine ni fursa za ukuzaji wa biashara mkoani Lindi, upanuzi wa
makazi, ongezeko la mahitaji ya umeme, fursa za kampuni za ulinzi na
uanzishwaji wa vyuo vya mafunzo mbalimbali ya taaluma zinazohitajika.
Pia kutakuwa na fursa kwa kampuni za ujenzi kwa ajili ya kazi
mbalimbali za ujenzi, uunganishaji vyuma, mahitaji makubwa ya vifaa vya
ujenzi ikiwemo saruji, vyuma, vifaa vya umeme na mengine.
Mradi huo pia utatoa fursa za huduma za forodha na uhamiaji, huduma
za viwanja vya ndege, uboreshaji wa bandari, huduma za benki, afya,
elimu, bima, kreni za kupandisha mizigo katika majengo marefu, huduma za
mawasiliano na zingine nyingi.
Mradi mwingine Mbali na mradi huo wa kusindika gesi, TPDC kupitia
ubia, inatarajia kuanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea katika Wilaya ya
Kilwa, kitakachohitaji uwekezaji mwingine wa dola za Marekani bilioni 2,
ambacho kitatoa ajira zingine 5,000.
Tayari TPDC imeshaingia mkataba na makampuni matatu ya Ferrostaal
Industrial Projects GmbH ya Ujerumani, Fauji Fertilizer ya Pakistan na
Haldor Topsoe ya Denmark, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Baada ya mkataba huo kwa mujibu wa taarifa hizo, TPDC na washirika
hao wataunda kampuni ya pamoja itakayoitwa Tanzania Mbolea and
Petrochemical Company (TMPC), ambayo itazalisha tani 2,200 za mbolea ya
ammonia kwa siku na tani 3,850 za mbolea ya urea kwa siku.
TPDC katika mradi huo kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo gazeti hili
linazo, itaanza kumiliki asilimia tano ya hisa kwa kutoa eneo lake la
ardhi na taratibu, itanunua hisa mpaka kufikia asilimia 40 ya hisa.
Mbolea ya mradi huo, inatarajiwa kuuzwa nchi za Afrika Mashariki na
Kusini mwa Ikweta, ambazo zimekuwa zikiagiza mbolea nje ya eneo hilo.
Tayari utafiti umeonesha kuwa kiwanda hicho kitakachotumia gesi
kuzalisha mbolea, kitakuwa na soko la bidhaa hiyo la nchini linalofikia
tani 204,527 za mbolea; Uganda tani 18,510; Kenya tani 276,878; Zambia
tani 200,411; Malawi tani 376,862; Madagascar tani 21,157; Afrika Kusini
tani 585,419 na Msumbiji tani 48,392.

0 comments:
Post a Comment