JESHI la Polisi mkoani Pwani limesema kuwa litaendesha operesheni
kubaini vijana wanaocheza mchezo wa ‘Pool’ kwani baadhi ya maeneo
unapochezwa mchezo huo ni vichaka vya kujificha wahalifu nyakati za
usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha,
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Bonaventura Mushongi alisema wahalifu hao
wamekuwa wakitumia mchezo huo kujificha huku wakisubiri muda ufike ili
wakafanye vitendo vya uhalifu.
Mushongi alisema wahalifu hao ambao hutumia muda mwingi kucheza
mchezo huo kama sehemu ya kupotezea muda, kwani baadhi ya wamiliki
huruhusu mchezo huo kuchezwa kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane.
“Inapofika usiku wa manane wahalifu hao ndio huondoka na kuelekea
kwenye maeneo ambayo wanayafanyia uhalifu ambako watu wanakuwa tayari
wameshalala,” alisema Mushongi.
Alisema wameshabaini maeneo hayo pamoja na kwenye baadhi ya baa
ambazo zimekuwa zikikiuka taratibu za kisheria kwa kufanya biashara
zaidi ya saa 5:00 usiku ambao ndio muda wa kufungwa kisheria.
“Tutahakikisha tunawafuatilia na kuwakamata wahalifu hao na wamiliki
wa maeneo hayo wanapaswa kuzingatia sheria kwa kufuata masharti ya
leseni na siyo kwenda kinyume kwani hatua zitachukuliwa kwa wale
watakaobainika kukiuka sheria hizo za biashara zao,” alisema Mushongi.
Aidha alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa jeshi lake ili
kwa pamoja waweze kukabiliana na wahalifu, kwani wakati mwingine
wanakwama kuwakamata kutokana na wananchi kushindwa kutoa taarifa juu ya
watu hao, licha ya kwamba wao wanawafahamu kwani wanatoka ndani ya
jamii.
0 comments:
Post a Comment