KATIKA kukabiliana na madereva wa pikipiki wanaopakia abiria zaidi ya
mmoja maarufu mshikaki, Jeshi la Polisi mkoani Pwani litatumia mbinu
mpya ya kuwapiga picha madereva hao na kuwakamata baadaye wakiwa kwenye
vituo vyao.
Jeshi hilo litatumia mbinu hiyo ili kuepusha ukamataji kwa
kuwakimbiza wale wanaofanya hivyo kwa lengo la kuepuka kusababisha ajali
wakati wa kuwakamata madereva hao wanaobeba mshikaki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha,
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bonaventura Mushongi alisema kuwa mbinu
hiyo itasaidia kuwabaini na kuwapiga faini kwa mujibu wa sheria.
“Tumeona tufanye hivyo kwani ukamataji wa zamani wa kufukuzana siyo
mzuri, unaweza ukasababisha ajali kwa wanaotumia pikipiki hiyo na hata
kugonga watu au mali katika kukwepa mkono wa sheria lakini kwa kuwapiga
picha tutawatafuta na kuwakamata wakiwa hawana abiria,” alisema.
Alisema mbali ya kukamata madereva bodaboda wanaobeba mshikaki ambayo
ni kinyume cha sheria, pia watawakamata kwa makosa mengine kama vile
leseni, kutokuwa na kofia mbili ngumu na kutozingatia sheria za
uendeshaji na usalama barabarani.
“Pia tunawaomba waendesha bodaboda watupe ushirikiano katika kubaini
wahalifu ambao wamekuwa wakitumia usafiri huo kufanikisha wizi hivyo
wanapaswa kutupa taarifa za watu wanaopanga kwenda kufanya uhalifu
kutumia vyombo hivyo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa endapo madereva hao wa bodaboda watatoa
ushirikiano kwa polisi itasaidia sana kukabiliana na uhalifu ambao
umekuwa ukijitokeza mara kwa mara.
“Pia kuna taarifa kuwa baadhi ya waendesha bodaboda nao wanajihusisha
na uhalifu, tunawataka waache vitendo hivyo kwani wao ni watoa huduma
na endapo watabainika kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa jeshi lake litashirikiana na viongozi wa bodaboda
katika kuhakikisha kuwa wanafuata sheria na kupambana na uhalifu na siyo
wao kuwa chanzo cha uhalifu na kuvunja sheria.

0 comments:
Post a Comment