Wednesday, January 6, 2016




 
 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani 
ametoa siku 14 kwa mgodi wa dhahabu wa Buckreef kuanza uzalishaji ama sivyo  wataandikiwa hati ya makosa na Afisa Madini Mkazi katika mkoa wa Geita.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada  ya kufika katika mgodi huo uliopo katika kata ya Lwamgasa mkoani Geita na kuona hakuna shughuli zozote za uzalishaji zinazoendelea.

“Najua kuwa hamjazalisha dhahabu mpaka sasa, lakini lazima mzalishe ili kulipa kodi na mrabaha, bila kufanya hivyo ndani ya siku 14 zijazo mtaandikiwa hati ya makosa kama sheria ya madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza, mgodi huu mnaumiliki toka mwaka 2011, lazima muanze uzalishaji,” alisema Kalemani.

Aidha Naibu Waziri alisema kuwa mgodi huo umechukua maeneo makubwa ya uchimbaji madini lakini hawayatumii, hivyo wayaainishe maeneo wanayohitaji kutumia na mengine wapewe wachimbaji wadogo.

Akijibu suala la ugawaji wa maeneo kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzam2000 inayomiliki mgodi huo kwa ubia na  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Joseph Kahama alisema kuwa wako tayari kukaa na Ofisi ya Madini mkoani Geita na STAMICO ili kuainisha maeneo watakayowaachia wachimbaji wadogo.

Kutokana na hilo Naibu Waziri alimwagiza Afisa Madini Mkazi  mkoa wa Geita, Mhandisi Laurian Rwebembera kukaa na watendaji wa mgodi huo tarehe 10 mwezi huu ili kuainisha maeneo hayo na kisha wayagawe kwa wachimbaji wadogo.

0 comments:

Post a Comment