SERIKALI iko katika mazungumzo na viwanda vyote vinavyozalisha sukari
kuangalia namna ya kuviondolea baadhi ya gharama za uzalishaji ili
bidhaa hiyo ishuke bei.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema
hayo jana alipofanya ziara katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera na
kuzungumza na uongozi pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Alisema wanalenga kuondoa gharama zisizo za lazima ili kupunguza bei
ya sukari ambayo imeonekana kuwa kero kwa wananchi. Alisema Serikali
ikiishakaa na wadau na itatoa jibu la kuridhisha kwa wananchi kwa maana
ya kuwapa bei itakayowaridhisha na kwenda na hali halisi ya uchumi wa
sasa.
Aidha Waziri Mwijage alisema ameridhishwa na uzalishaji unaofanywa na
kiwanda hicho na akasema ni mfano wa kuigwa. Meneja wa Kiwanda hicho,
Ashwin Lana alisema kimeajiri wafanyakazi 600 huku zaidi ya 400 wakiwa
wa kudumu.
Wakati huo huo, wazalishaji, watumiaji wa sukari ya viwandani na ile
ya matumizi ya nyum bani pamoja na wadau wote wa sukari nchini, wamepewa
siku sita kupeleka taarifa za kiasi za sukari walichonacho kwenye
hifadhi zao, ili kuhakikiwa kabla ya msimu wa kufunga viwanda haujaanza.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana kwa vyombo vya habari na Bodi
ya Sukari nchini (SBT), wahusika hao wanapaswa kuwasilisha taarifa zao
kabla ya Januari 11, mwaka huu.

0 comments:
Post a Comment