BENKI Kuu (BoT) imeitoza faini Benki ya Stanbic Sh bilioni tatu baada
ya kubaini benki hiyo imefanya miamala ya kutia shaka inayohusu malipo
kwa kampuni ya Kitanzania ya EGMA ya Dola za Marekani mil.6
zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo na kutolewa ndani ya muda
mfupi.
Stanbic iliwezesha Serikali ya Tanzania kuuza hati fungani za dola
milioni 600 (Sh trilioni 1.3) kwa benki ya Standard Chartered ya
Uingereza. Mauzo hayo yalifanyika mwaka 2012 kwa Serikali kwa masharti
ya kulipwa riba ya asilimia 1.4; lakini Stanbic tawi la Tanzania
iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya Serikali ya Tanzania kutakiwa
kulipa riba ya asilimia 2.4.
Adhabu iliyotangazwa jana na Serikali kwa benki hiyo, inatokana na
Stanbic kuilipa EGMA Dola za Marekani milioni 6 ambazo ziliingizwa
kwenye akaunti ya kampuni hiyo ya kitanzania na kutolewa kwa muda mfupi
kwa njia ya fedha taslimu, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za
kibenki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philipo Mpango alisema BoT katika uchunguzi wake, imebaini malipo hayo
kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki
na yalihusisha uongozi wa Benki ya Stanbic.
Dk Mpango alisema BoT imechukua hatua ya kutoza faini benki hiyo kama
onyo iweze kuwa makini katika kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa
kwa mujibu wa taratibu za kibenki za kuzingatia sheria.
“Hatua hii ni onyo kwa benki na taasisi zingine za fedha
zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha taratibu za
kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema Dk Mpango.
Waziri alifafanua kuwa sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika siku 20 ambazo zitaisha Januari 30 mwaka huu.
“Endapo BoT haitaridhika na utetezi wake, Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo,” alisema.
Alisema hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya
fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na
sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Uchunguzi wa BoT
Akielezea hatua za uchunguzi huo, Dk Mpango alisema taarifa ya
uchunguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu
na BoT iliagiza bodi ya wakurugenzi ya benki kuchukua hatua stahiki za
kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Alisema benki hiyo pia iliagizwa kutoa taarifa kwa kitengo
kinachochunguza makosa ya fedha (FIU) kilichoko Wizara ya Fedha na
Mipango kuhusu miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama
sheria ya kuzuia utakatishaji wa fedha haramu inavyoelekeza.
“Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala hiyo iliyotiliwa shaka,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alisema ripoti hiyo ya BoT pia iliombwa kutumiwa na Shirika
la Upelelezi la Makosa Makubwa (SFO) katika kesi dhidi ya Benki ya
Standard ambayo waliruhusu itumiwe kwa kuzingatia chanzo cha ripoti
hiyo.
“Hatimaye Standard ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya
dola za Marekani milioni 32.20 na kiasi cha dola za Marekani milioni
saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania,” alisema Dk Mpango na kufafanua
kuwa dola milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola milioni moja ni riba.
Takukuru yawahoji
Akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao walitaka kufahamu
wahusika wengine wamechukuliwa hatua gani, Dk Mpango alisema bado
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea na
uchunguzi katika makosa yanayohusu rushwa.
“Hili ambalo limefanyika leo ni kuhusu uchuguzi wa BoT kuhusu masuala
ya miamala ya kifedha, sasa kuna vyombo vingine vya dola vinaendelea
kuwahoji wahusika na wakikamilisha kazi yao watatangaza hatua za
kuchukua,” alisema Dk Mpango.

0 comments:
Post a Comment