WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa kushirikiana na
Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Usalama wa Taifa wamekamata
madini yenye thamani ya jumla ya Sh milioni 11.2 ambayo yalikuwa
yakitoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA).
Aidha serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imesema inatoa
motisha kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa kwa Kamishna wa Madini ama
Wakala za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini
zitakazowezesha ukamataji wa madini.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TMAA, Yisambi
Shiwa alisema raia mmoja wa kigeni na Mtanzania, walikamatwa wakiwa na
madini hayo bila kuwa na kibali chochote cha usafirishaji kama ambavyo
Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza.
“Raia huyu wa kigeni ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za
kiuchunguzi kwani tayari ameshafunguliwa kesi mahakamani, alikuwa
anasafiri kwenda mji wa Bangkok Thailand na alikamatwa akiwa na madini
ya aina mbalimbali ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire, green
tourmaline, quartz na rhodolite,” alisema Shiwa.
Shiwa alisema tukio lingine, Mtanzania ambaye alikuwa anasafiri
kwenda Ujerumani alikamatwa akiwa na madini na kufikishwa katika vyombo
vya dola. Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi
Januari 13 mwaka huu, kumekuwepo na matukio 14 ya utoroshaji madini.
Alisema madini yenye thamani ya Sh bilioni 3.2 yalikamatwa na
wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika viwanja
vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza ambapo
yote yalitaifishwa na Serikali.

0 comments:
Post a Comment