
MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi (MUWSA), imetoa notisi ya siku 14 kwa taasisi za serikali ikiwamo ofisi ya kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, ambao ni wadaiwa sugu wa Ankara za maji, kulipa madeni yao vinginevyo watasitishiwa huduma...,
Muwsa inazidai baadhi ya taasisi za serikali zaidi ya Bil 1.2 kwa kipindi cha takribani miaka 7 ikiwa ni malimbikizo ya Ankara za maji jambo ambalo limechangia baadhi ya miradi ya mamlaka hiyo kutotekelezeka kwa wakati. Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Joyce Msiru alisema tayari bodi ya wakurugenzi wa mamlaka hiyo imefanya mazungumzo na taasisi hizo kuhusu ulipwaji wa deni hilo ingawa baadhi ya taasisi zimeonesha kushindwa kuyalipa.
Alizitaja taasisi hizo na kiasi kinachodaiwa kuwa ni ofisi ya kamanda wa polisi mkoani humo, Sh Mil 528.6, Shule ya mafunzo ya polisi Moshi (MPA) Sh Mil 401.9 na Magereza kiasi cha Mil 203.7 ambapo baada ya kumalizika siku 14 bila madeni kulipwa mamlaka itawakatia huduma.
“Bodi imezungumza na uongozi wa taasisi hizo, inaonekana uwezekano wa kulipa ni mdogo….ni raia ya mamlaka kwa serikali kuu isaidia kulipwa kwa deni hilo, hii itatusaidia kukamilisha miradi mingine na kusambaza huduma kwa wananchi wa kawaida”alisema.
Msiru alisema deni hilo limegawanyika katika makundi mawili, moja ni kwa taasisi wadaiwa sugu na nyingine ni taasisi nyeti ikiwemo hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi ambazo zinadaiwa kiasi cha Mil 130.2 ambazo nazo zimetakiwa kuongeza kasi ya kulipa madeni yao. Alisema taasisi nyingine za serikali tayari zimeshaingia makubaliano ya kumaliza madeni yao na kutaka kuondokana na mfumo wa kulipa nusu au robo ya fedha wanazodaiwa na badala yake walipe kwa wakati fedha halisi zinazodaiwa.
Alizitaja taasisi nyingine zinazodaiwa ni pamoja na shule ya sekondari ya ufundi Moshi,(Moshi Technical), Mil. 34,Shule ya sekondari Old Moshi Mil. 17 na taasisi ya mahakama Moshi zaidi ya Mil. 6 ambazo amehimiza kulipwa kwa madeni hayo
.
“Niwashukuru sana wakazi wa manispaa ya Moshi kwani wamekuwa wasikivu na wanalipa Ankara zao za maji kwa wakati na kila mwezi, tunapata shida na taasisi za serikali hususan wale wenye madeni sugu tunaomba ili tuweze kufikia malengo yetu taasisi hizi zitusaidie kumaliza madeni yao” alisema.
Aidha mkurugenzi huyo alisema kwa kipindi cha mwaka 2013/14 baadhi ya miradi inayotekelezwa na mamlaka hiyo ilishindwa kufanyika kutokana na fedha nyingi za mamlaka hiyo kuwa kwa taasisi hizo.
0 comments:
Post a Comment