HOJA SI UKUBWA WA BARAZA, HOJA NI UKUBWA WA GHARAMA ZA KUENDESHA SERIKALI
Nimefuatilia jinsi ambavyo hoja yangu niliyoitoa juzi kwa nia njema
ilivyojadiliwa nchini kwa kuungwa mkono na wengi na wengine kuipinga.
Mimi nadhani hoja yangu isijadiliwe au kukanushwa kisiasa, bali iangaliwe tu kiuhalisia ili kusaidia Serikali ya Rais Magufuli.
Mimi nadhani hoja yangu isijadiliwe au kukanushwa kisiasa, bali iangaliwe tu kiuhalisia ili kusaidia Serikali ya Rais Magufuli.
Aidha najua sana kwamba katibu mkuu siyo mjumbe wa baraza la mawaziri.
Lakini najua vile vile kwamba jina au cheo tu cha uwaziri si kila kitu
kwenye kupunguza gharama za kuendesha serikali. Gharama za kuendesha
serikali ni idadi ya mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wa idara
mbalimbali za serikali, na gharama zingine za kuendesha idara zao.
Na wala sijapinga mazuri anayofanya rais hadi sasa. Mbona pale rais
alipofanya vizuri tumempongeza? Kwa mfano kutumbua majipu ambayo
yaliivishwa tayari na serikali ya awamu ya nne. Vile vile alipopunguza
idadi ya wizara na idadi ya mawaziri kutoka 29 kufikia 19 mbona
tulipongeza? Na hapa tuliamini ni mwanzo wa kupunguza ukubwa na gharama
za kuendesha serikali. Nasema mwanzo kwa sababu ukubwa na gharama za
kuendesha serikali si kupunguza tu idadi ya wizara na mawaziri, bali
kupunguza pia idadi ya makatibu wakuu ili kulingana na idadi ya
wizara....ni kupunguza na kuunganisha idara mbalimbali za serikali na
wakurugenzi wake. Ukifanya hivyo ndiyo unapunguza gharama za kuendesha
serikali. Na hii ndiyo ilikuwa ahadi ya Magufuli kwenye kampeni.
Lakini kama ameona kwamba kuleta ufanisi serikalini lazima ajaze
watendaji wengi kwenye wizara, kama anavyoendelea kufanya, aseme tu
hivyo, lakini akijua hatua hiyo haitapunguza gharama za kuendesha
serikali ambazo wabunge, hasa wa upinzani, wamekuwa wakipigia kelele
kwenye serikali ya awamu ya nne.
Hata hivyo hili la kuleta
ufanisi pamoja na kuteua makatibu wakuu wengi wanaoonekana wazuri kwa
utendaji, kuna wizara ambazo hakushauriwa vizuri na akateua makatibu
wakuu wale wale na kuwarudisha pale pale wakati walikuwa "mizigo" na
walikwamisha mno sekta husika katika awamu ya nne. Hawa ni watu ambao
rais au katibu mkuu kiongozi angeenda kwenye wizara zao leo na kuitisha
kura ya siri ya wakurugenzi na wafanyakazi wote, asilimia 90 ya
watumishi wote wangewakataa makatibu wakuu hao. Ni heri kukosea kuteua
kwa mara ya kwanza kuliko kukosea kuteua "mizigo" iliyokuwepo.
Tukirudi kwenye hoja ya msingi ya gharama za kuendesha serikali,
nimesema na ninarudia kusema: bila kutakiwa kutoa takwimu hapa, gharama
za waziri mmoja na ofisi yake ni ndogo sana kulinganisha na gharama za
katibu mkuu mmoja na ofisi yake, kwani waziri tayari analipwa sehemu
kubwa ya mshahara na marupurupu kutokana na yeye kuwa mbunge (na hapa
niwajuze baadhi ya walionipinga kwamba waziri halipwi mishahara miwili -
ya ubunge na ya uwaziri).
Na hapa hatujajadili mikanganyiko
mingine ambayo haijawekwa wazi hadi sasa. Kwa mfano kutakuwa na afisa
masuhuli mmoja wa wizara au maafisa masuhuli wawili au watatu kwenye
baadhi ya wizara? Kwa kawaida wizara inakuwa na fungu (vote) moja; sasa
katika hali hii kila idara ya wizara itakuwa na fungu (vote) tatu
(ukiacha idara zinazojitegemea)? Je hili la afisa masuhuli mkuu wa
wizara kutokuwepo haitaleta shida katika uwajibikaji? Na vipi katika
kusimamiwa na bunge na kamati zake? Nani hasa mtendaji mkuu wa wizara
atakayewajibika kwa bunge kwa mambo ya kisera ya wizara nzima? Wote
watatu?
Hatua hii ya rais magufuli ya kuwa na makatibu wakuu wa
vitengo (na siyo wa wizara) ingesubiri hoja ya kikatiba ya mawaziri
kutokuwa wanasiasa (wabunge) ili wawe watendaji wakuu na wawajibikaji
wakuu wa wizara (cabinet secretaries) kama ilivyo nchi ya jirani ya
Kenya.
Lakini kwa sasa ningeshauri hoja hii iahirishwe halafu
turudi tena kuijadili baada ya "taasisi" ya makatibu wakuu wapya
kupangwa - kwa maana ya kila mmoja kupangiwa idara na wakurugenzi chini
yake (na ninahisi kutakuwa na nyongeza ya idara). Na baada ya hapo
uchambuzi wa gharama za kuendesha serikali hii ufanywe na ulinganishwe
na gharama za uendeshaji wa serikali ya mwisho ya JK ambayo tayari
ilikuwa inalalamikiwa kwa ukubwa wake.
Dr. Milton Makongoro Mahanga

0 comments:
Post a Comment