Mamlaka ya Uhifadhi Selous (Selous Conservation Authority )
Zitto Kabwe
Nimeamka mapema asubuhi katika lodge ya Mivumo inayoendeshwa na Serena Hotels. Kambi hii iliyo katikati ya pori la akiba la Selous, ndio makazi yangu kwa siku mbili za mapumziko ya mwisho wa mwaka 2015 na mwanzo wa mwaka 2016. Niliamka mapema tayari kwenda kuona wanyama katika siku yangu ya pili baada ya kutumia siku ya kwanza kutembea kuona wanyama wa mtoni, mto Rufiji.
Ilinichukua kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa tisa mchana kuweza kuona tembo. Kundi dogo lililokuwa na tembo kama watano hivi lilijitokeza mnamo saa tisa na nusu jioni, tena wakiwa na wasiwasi mkubwa. Hii ni tofauti kabisa na matembezi yangu yaliyopita katika maeneo mengine kama vile, Hifadhi ya Ruaha ambapo niliona makundi ya tembo takribani kila mahala. Ni tofauti hata na watu wanaopita barabara ya Mikumi ambapo hubahatika kuona tembo.
Namwuliza mwongozaji wetu, ananiambia kuwa ujangili umeathiri sana Pori la Selous (Selous Game Reserve – SGR). Mpaka tunarudi kambini kwetu, Mivumo Lodge, nilibahatika kuona tembo wasiozidi 8. Wanyama wengine pia hawakuwa kwenye makundi makubwa. Hata Nyumbu na Pundamilia walikuwa kwenye makundi ya wanyama wachache wachache sana.
Katika kipindi cha miaka 5 Selous ilipoteza 67% ya tembo wake. Nimeshuhudia ukame wa tembo katika hifadhi ambayo ndio ilikuwa na idadi ya tembo wengi zaidi katika bara la Afrika. Katika ujangili wa kuua tembo wanyama wengine wanaathiriwa na milio ya risasi kutoka kwenye magobore ya majangili.
Mto Rufiji unapita ndani ya SGR. Eneo maarufu la Stigler’s Gorge, lenye uwezo wa kuzalisha 2000MW za umeme zipo ndani ya Pori hili la Akiba. Jioni ya kwanza ya siku zangu mbili (siku ya mwisho ya mwaka 2015 ) niliendeshwa kwa boti juu ya Mto Rufiji. Mto huu ni muunganiko wa mto Kilombero na mto Ruaha na humwaga maji yake kwenye bahari ya Hindi. Niliweza kuona viboko na mamba wengi. Kipindi hiki ni kipindi cha mamba kuzaliana na niliweza kuona mayai ya mamba yakitotolewa na kuona watoto wa mamba. Eneo la Stigler’s gorge maji yake yanaenda kwa kasi sana hatukuweza kufika kwa boti. Mamba na viboko wa Selous ni wakubwa.
Niliambiwa Selous kuna Faru na Chui. Hatukuweza kuona chui japo naambia ni pori lenye chui wengi zaidi kuliko hifadhi zote nchini. Tuliona Simba na katika tukio moja la kusikitisha tuliona watoto 2 wa Simba waliouwawa katika kichaka kimoja. Katika wanaoitwa The Big 5, tuliona Nyati, Simba na Tembo. Faru wamekuwa katika hali mbaya sana ya kutoweka kabisa kwa sababu ya ujangili. Inasemekana wamekwisha kabisa, hatari ambayo tembo wa Selous wanaikaribia.
Pori la Akiba la Selous ni kubwa sana. Usimamizi wake kupitia idara ya Wanyamapori na sasa Mamlaka ya Wanyamapori sio madhubuti kwa sababu idara haina vifaa vya kutosha wala askari wanaotosha kudhibiti ujangili. Tofauti na wenzao wa TANAPA, askari wa idara ya Wanyamapori hawalipwi vizuri, hawana vifaa kama magari na maboti wala hawana bima ya maisha yao. Mtandao wa majangili ni mkubwa na umesheheni vigogo kwenye siasa, biashara na hata vyombo vya usalama. Tunahitaji kufikiria upya namna ya kuilindi hazina hii ya nchi yetu.
Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilometa za mraba 55,000 hivi. Kwa maana hiyo Selous ina ukubwa sawa sawa na 5.8% ya ukubwa wa Tanzania nzima. Unaweza kuzichukua nchi za Rwanda na Burundi, zote kwa pamoja, ukaziweka ndani ya Selous na eneo linguine likabaki. Kwanini tuone Selous kama Hifadhi au Pori lingine lolote? Uendeshaji wake ni lazima uwe tofauti, kama ilivyo Ngorongoro sasa na faida zake tunaziona.
Tungeanzisha Selous Conservation Authority ( Mamlaka ya Selous ) yenye bodi yake na uendeshaji unaojitegemea ikiwemo kutangaza utalii. Selous inaweza kuunganishwa vizuri kiutalii na Kilwa au hata Zanzibar na kuingiza mapato mengi ya fedha za kigeni na kutimiza lengo la kulinda urithi huu adimu. Kutokana na ukubwa wa eneo, Selous yaweza kugawanywa sehemu mbili, moja ya utalii tu na kupiga marufuku uwindaji ( kama 35,000sqkm ) na eneo linguine kwa ajili uwindaji utakaosimamiwa na kudhibitiwa na Mamlaka ya Selous kwa ufanisi mkubwa. Mamlaka ya Wanyamapori inaweza kusimamia mapori mengine ya akiba tofauti na Selous

0 comments:
Post a Comment