Wednesday, February 3, 2016

(Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi)
Wiki iliyopita helikopta ya doria iliyokuwa ikifanya kazi kwenye Pori la Akiba la Maswa mkoani Simiyu ilishambuliwa na majangili na kumuua kwa risasi rubani wake, Rodgers Gower.
Tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiongeza nguvu kwenye vita dhidi ya majangili ambayo yanatishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama kama tembo, ambao ndovu zake ni nyara zenye thamani kubwa duniani.
Bila shaka tukio la kuuawa kwa rubani wa helikopta hiyo limeanza kutuaminisha kwamba shughuli hiyo ya ujangili sasa inafanywa kijeshi na kwa kutumia wataalamu.
Kwa maneno mengine, tukio hilo linatuma ishara kwamba vita dhidi ya ujangili si lelemama kwa kuwa sasa haifanywi na watu wenye njaa tu ya fedha, bali watu wenye utaalamu wa hali ya juu na wanaoweza kupambana na yeyote anayejaribu kuwaharibia biashara yao.
Na kwa maneno mengine ni kwamba juhudi zinazofanyika hadi sasa ni za kupambana na dalili tu na si mzizi wenyewe wa ujangili, ambao ni mtandao unaohusisha watu wengi wa sehemu tofauti; kuanzia wanakijiji wa vijiji vinavyozunguka mbuga na hifadhi zetu, watendaji wizarani, polisi, hadi wanasiasa.
Ndiyo maana tembo wanauawa na pembe zao kuhifadhiwa hadi mzigo unapotosha na kusafirishwa kutoka mbugani au kwenye hifadhi hadi Uwanja wa Ndege au bandarini na pengine hata kufanikiwa kupitishwa, bila ya wasafirishaji au wauaji kung’amuliwa.

Hiyo ina maana kwamba si wanakijiji wanaostukia harakati hizo za kukusanya pembe za ndovu, wala askari wa Idara ya Wanyamapori, wala polisi wanaokagua mizigo wanayoishuku, wala maofisa walio bandarini au uwanja wa ndege ambao wanafanikiwa kukamata mizigo hiyo hadi inatoka nje ya mipaka.

Huu ni mtandao mkubwa na wenye nguvu ambao unahitaji juhudi za ziada kuusambaratisha.

Kwa hiyo, vita dhidi ya ujangili haitakiwi iwe ya maneno mepesi, bali iwe inayoonyesha ugumu uliopo na ni jinsi gani umma unavyoweza kushiriki kupambana nao.

Vita hiyo inahitaji mkakati mkali ambao malengo yake yawe ni kuungamiza mtandao wa ujangili na si kupunguza vitendo hivyo kwa sababu kama majangili wameanza kupata ujasiri wa kushambulia kwa silaha kali watu wanaojaribu kuwadhibiti, ni dhahiri kuwa wameingia vitani na hawataki mchezo tena.

Ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuchukulia tukio la kuuawa kwa rubani huyo kuwa mwanzo wa kuung’amua mtandao wa majangili na kukusanya taarifa nyingi kabla ya kuanza vita ya kupambana na uovu huo. Kukiwa na nia ya dhati, ujangili utaangamizwa. 

0 comments:

Post a Comment