JINA la Songea limekuwa maarufu kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kudhani kuna mkoa unaitwa Songea.
Ukweli ni kwamba Songea ni wilaya iliyopo katika mkoa wa Ruvuma na jina
hilo linatokana na shujaa wa Wangoni, Nduna Songea Mbano. Ni vigumu
kuilezea historia ya vita ya Maji Maji bila kutaja jina la Songea,
shujaa huyo wa Wangoni kutokana na mchango wake mkubwa katika kupigania
haki na uhuru wa Waafrika.
Songea alikuwa mtu mwenye sifa ya
kipekee kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya kazi bila kuchoka na
katika mazingira magumu . Aliwashirikisha wananchi wake katika kufanya
maamuzi na kujijengea mazingira yaliyomfanya kila mtu amuamini,
kumsikiliza na kumheshimu.
Nduna Songea Mbano alikuwa ni shujaa
aliyesimama kidete na kupinga hoja ya utawala wa Kijerumani ambao
ulionekana wazi unataka kudhalilisha utawala wa kabila la Wangoni.
Songea alisimama kidete na kusema waziwazi kuwa kuwa Wangoni hawawezi
kuutambua utawala mpya wa kijerumani.
Hivyo kutokana na ujasiri
wake, baada ya wajerumani kuwashinda vita kwa taabu dhidi ya Wangoni
,jina lake hilo likapewa hadhi ya mji wa Songea badala ya jina halisi la
‘Ndonde’ mwaka 1906. Kiongozi huyo alikuwa ni miongoni mwa wasaidizi (
Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la Wangoni (Nkosi) Chifu Mputa bin
Gwezerapasi Gama.
Wasaidizi wengine ni Mgendera Mawaso Gama,
Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba Mbano, Mtekateka
Muyamuya Tawete na Fratela Fusi Gama. Wasaidizi wake wengine wa Chifu
Mputa ni pamoja na Nduna Maji ya kuhanga Komba, Zimanimoto Gama,
Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna Mkomanile ambaye
alikuwa ni mwanamke pekee kuwa na wadhifa huu wa Uduna.
Nduna
Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake na hata chifu
Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza Manduna wenzake na
wapiganaji wa vita ya Maji Maji. Ofisa Elimu Msaidizi wa Makumbusho ya
vita ya Maji Maji ya Songea, Erick Soko , anaelezea sifa za ziada
alizokuwa nazo Nduna Songea katika kuongoza vita vya Maji Maji dhidi ya
wakoloni wa kijerumani.
Soko anayaelezea maisha ya Songea kuwa
alitokea kupata umaarufu mkubwa ikilinganisha na wenzake 11 kwa kuwa
alikuwa na ueledi na ustadi wa kuandaa mikakati ya kivita, na kutoa
maamuzi mazito yasiyotetereka na kuyasimamia kikamilifu. Umakini wake
mkubwa ni kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo
hili ulianza kujitokeza julai 12, mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani
kwa Mkuu wa Wilaya wa Kijerumani, Luteni Engelhardt.
Soko
anaeleza kuwa rekodi zilizopo zinaonyesha tarehe hiyo alionekana kuwa ni
mtu wa kipekee katika idadi ya Manduna 11 waliokuwa wasaidizi wa Chifu
Mputa Gama . Hatua hiyo ilitokana na kitendo chake cha kubisha wazi wazi
tamko la utawala mpya wa Wajerumani la kuwataka wangoni wakomeshe
biashara ya utumwa.
Kwa mujibu wa Soko, siku hiyo ilikuwa ni siku
rasmi ambayo utawala wa kikoloni ulikuwa unaanzishwa kwenye mji wa
Ndonde , wakati huo kabla ya kuitwa mji wa Songea. Mji wa Ndonde katika
mkoa wa Ruvuma ulikuwa chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la
Kijerumani, alikuwa ni Mkuu wa Kanda ya Kusini.
Hivyo anasema,
wakati Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao maeneo ya ukanda wa
kusini walikumbana na msuguano mkubwa kutoka kwa tawala za Kiafrika hasa
utawala wa Wangoni. Soko anasema , wangoni walikuwa na tabia ya kwenda
mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na kuwaleta Songea
kuwafanyisha shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.
Hata hivyo anasema , tabia hii ya Wangoni iliwachukiza Wajerumani, ambao
walikuwa wanaheshimu makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Berlin
wa mwaka 1884 hadi 1885. Soko anasema makubaliano hayo yaliyofikiwa ni
kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima ikomeshe biashara ya
utumwa na nyakati hizo Wajerumani walikuwa wamejiimarisha katika mikoa
ya Lindi na Mtwara.
Hata hivyo anasema, Wajerumani walipofika
Ruvuma wakatoa tamko kwa Wangoni haitaruhusiwa tena kwenda Lindi, Mtwara
na maeneo mengine kuchukua mateka na mateka wote waliochukuliwa
waachiwe huru ili kukomesha biashara ya watumwa. Hivyo anasema , baada
ya Wajerumani kutoa tamko hili ndipo Nduna Songea Mbano alipojitokeza
waziwazi na kusimama na kuipinga hoja ya Wajerumani kuhusiana na tamko
hili.
“Songea alipinga hoja hiyo mbele ya utawala wa Kijerumani
akisema utawala wa kabila la wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na
msimamo wao ni kutoutambua utawala mpya wa kijerumani na tamko lao,
”anaelezea Soko. Kwa mujibu wa Kiongozi huyu wa Wangoni ujio wa utawala
wa Wajerumani ulikuwa na lengo la kudhoofisha utawala wa Machifu na
Manduna katika maeneo yao.
Historia inaeleza kuwa Wangoni waliona
kufuata kanuni za Wajerumani, watapoteza mila za kitamaduni za Wangoni.
Kutokana na msimamo wa Nduna Songea Mbano , kuanzia hapo Wajerumani
walimuona kuwa ni mtu hatari katika utawala wao mpya na walimuweka alama
maalumu na kuanza kumfuatilia nyendo zake.
Misimamo yake hiyo
ilizidi kujenga umaarufu mkubwa na matamshi yake mbele ya Wajerumani
kuwa yupo tayari kwa lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za
kiafrika zinadharauliwa na wakoloni kwa namna yoyote ile. “Songea
alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wake wawe na umoja,
upendo na mshikamano na kila anapotoa maelekezo wafuasi wake
wanayatekeleza kwa umakini na kwa ukamilifu,” anaelezea Soko.
Ili
kuonesha alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa uweledi mkubwa bila
kusaliti dhamira yake , mwanzoni mwa mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi
lake la kupambana na utawala wa Wajerumani. Hatua ya kwanza aliwachukua
watu wake na kuwapeleka katika mlima wa Chandamari uliopo kati kati ya
mjini na kufanya nao mkutano ulioendana na kutoa mafunzo ya kivita na
kuwajengea ujasiri wa kuwachukia Wajerumani.
“ Wakiwa kwenye
mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina madhara ya kuukubali utawala wa
Wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi wake ya kuwaondoa Wajerumani kwa
lazima.” Soko anaelezea . Songea Mbano aliwafahamisha wafuasi wake ya
kwamba eneo hilo ni mali yao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya
utawala wao , inakuwaje waletewe utawala mpya wa Wajerumani wakati
hawauhitaji.
Hata hivyo mnamo Julai 13, 1897, utawala wa
Wajerumani waliamua kuwaalika machifu na manduna wote Bomani kwa Mkuu wa
Wilaya wa kwanza katika eneo la ungoni. Amri ya kualikwa kwao ilitolewa
na Mkuu wa Jeshi la Wajerumani katika eneo la ungoni, Luteni Engelhardt
.
Machifu na manduna wa Wangoni waliambiwa mtu yeyote katika
eneo lake atakayekaidi amri yoyote kutoka kwa uongozi mpya wa Wajerumani
atapigwa risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha . Katika
kuwatisha watakaokaidi amri ,machifu na manduna walichukuliwa hadi
katika mlima wa kulenga shabaha unaojulikana ‘ Mlima Chandamari’ uliopo
kati kati ya mji wa Songea.
Walipofikishwa hapo Wajerumani
walionesha nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi katika mwili wa
binadamu na kwamba silaha za kijadi na kimila za wangoni haziwezi kufua
dafu mbele ya silaha zao. Licha ya Wajerumani kutoa vitisho vingi, Nduna
Songea Mbano aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa kuuchukia
utawala wa Wajerumani na kuutetea utawala wa Kiafrika mpaka ilipotokea
vita ya Maji Maji.
Wakati huo , Nduna Songea Mbano alikuwa
amejificha kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa chandamari na
usiku akiwa anakutana na askari wake nje ya pango hili na kuwapa mafunzo
zaidi ya kivita. Hata hivyo anaelezea kuwa, wakati mapigano yakiendelea
Wajerumani walianza kumtafuta Nduna Songea Mbano ili wamkamate kwa
lengo la kufanya naye mazungumzo ya maridhiano.
Katika vita hii
Nduna Songea Mbano alitoa ushindani mkubwa kwa Wajerumani na alionesha
ustadi mkubwa kwenye mapigano na sehemu zote ambazo Wajerumani
walipigana. Hivyo anaeleza kuwa, Wajerumani walipoona wanaendelea kupata
madhara makubwa kutokana na vita hivi waliamua kuwakamata ndugu na
familia ya Nduna Songea Mbano.
Waliomakatwa ni pamoja na Chifu
Mputa Gama na Manduna wengine ambao walifungwa gerezani likiwa ni lengo
la kumdhoofisha Nduna Songea Mbano. Baada ya kumdhoofisha nguvu ya jeshi
lake , Nduna Songea Mbano aliamua kutoka kwenye pango alikojificha na
kwenda kwa Wajerumani ili kutaka watu wake waachiwe huru.
“
Hakufua dafu katika mpango huu, naye alikamatwa na kuwekwa gerezani na
Wajerumani waliamua kuwahukumu wafungwa wote kunyongwa hadi kufa akiwemo
chifu wa kabila la Wangoni Mputa Bin Grazerapasi Gama,” anaeleza Ofisa
Elimu huyu. Katika jambo la kusikitisha, Ofisa Elimu Msaidizi wa
Makumbusho haya anasema kuwa, wafungwa hawa waliamuliwa kuchimba shimo
kubwa bila kujua shimo hilo ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao. “
Ilipofika siku ya kunyongwa walinyongwa kwa zamu siku mbili na maiti zao
kwenda kuwekwa kwenye kaburi walilokuwa wamelichimba wakiwa hai hadi
wote 66 na kuzikwa kwa pamoja kwenye kaburi “ anaelezea Ofisa Elimu
huyu. Hata hivyo Wajerumani walimuachia Nduna Songea Mbano aweze
kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi wakiamini kuwa yeye ni
kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na hivyo kusikilizwa vizuri.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria zilielezwa na Ofisa El. |
0 comments:
Post a Comment