Wednesday, March 23, 2016

Wakati matukio ya uhalifu wa kutumia silaha yakizidi kupamba moto nchini, Rais John Magufuli amesema ni aibu kwa polisi kunyang’anywa silaha na majambazi na kwamba wanazopewa ili kulinda si za maonyesho.
Akizungumza baada ya silaha zake mbili kukaguliwa na polisi nyumbani kwake, Ikulu jijini Dar es Salam jana, Rais Magufuli alisema: “Mfanye kazi bila woga. Ni aibu kumwona askari polisi mwenye silaha ananyang’anywa silaha na silaha anayo.
“Ni aibu na nasema hiyo ni aibu,  mpaka jambazi akunyang’anye silaha na wewe una silaha halafu unakwenda unaripoti juu kwa OCD, RPC, nimenyanganywa silaha na wewe uko mzima na silaha imeondoka ni aibu kwa jeshi la polisi.
 “Hili mlisimamie hakuna kunyang’anywa silaha sasa, ndivyo tulivyofundishwa, na ndiyo maana mnapewa silaha kulinda, huwezi ukapewa silaha  ya kulinda ya maonyesho, maonyesho yapo gallery, lakini ukishapewa silaha mtu akicheza nayo lazima uliye nayo, najua umenielewa Kamanda (Simon) Siro (Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam).” 
  
Kuhusu ukaguzi wa silaha, Rais Magufuli alisema ameamua kutekeleza wajibu wake kama ambavyo iliagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kutaka watu wote wenye silaha kuzihakiki.
 
KAMANDA SIRO
Kwa upande wake, Kamanda Siro aliwataka watu kuitikia wito kuhakiki silaha zao bila kusubiri nguvu itumike kuzitafuta zilipo.
“Wazalendo wataitikia kwa uzuri tu na wanaofikiri watabaki nazo tunaitelijensia kali tutawakamata, kama unasialaga za kivita rudisha,” alisema Kamanda Siro.
 
Silaha za sitaki shari zilipookotwa
Aliyekuwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Julai 20 mwaka juana, alisema Julai 19, jeshi hilo lilipata habari za kuaminika juu ya silaha zilizoporwa Kituo cha Sitakishari; kufichwa Mkoa jirani wa Pwani zikiwa porini katika eneo lisilofahamika vizuri.
 
Kundi kubwa linaloundwa na vikosi mbalimbali vya polisi, lilienda mkoani humo na kufanya msako katika kijiji cha Mandimkongo, wilayani Mkuranga katika msitu, kikosi hicho kilifukua kwenye shimo na kupata bunduki 15 kati ya hizo, saba aina ya SMG, saba SAR, magazine moja ya SMG na risasi 28.
 
Kamishna Kova alisema kati ya silaha zilizokamatwa, 14 ni za Kituo cha Sitakishari na mbili za majambazi wenyewe, ikiwamo silaha moja aina ya Norinko ambayo inafanyiwa uchunguzi ili kujua iliibwa wapi.
 
Katika shimo hilo pia zilipatikana fedha taslimu za Tanzania sh. milioni 170 ambazo zilifungwa kwenye sanduku maalumu ambapo Kamishna Kova aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kulitokomeza kundi linalovamia vituo vya polisi, kuua askari, kupora silaha kwa kutumia usafiri wa pikipiki.
 
Aliongeza kuwa, jeshi hilo linawatafuta watu wengine waliotajwa kwa majina ya Abdulazizi Abdulrashid au Ustaadhi Abdulaziz, mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni kiongozi wa kundi la wahalifu hao.
 
Polisi walionyang'anywa silaha
Januari 2015, kituo cha Polisi Ikwiriri kilivamiwa na majambazi ambako askari polisi wawili waliuawa, na bunduki tano zikaibiwa zikiwamo SMG mbili, SAR mbili, Shortgun moja na risasi 60.
 
Uvamizi mwingine ulifanyika Septemba 7 mwaka 2014, kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Bukombe, mkoani Geita, ambako majambazi yaliua askari wawili na kupora bunduki 10 aina ya SMG.
 
 Mnamo Juni 12, 2014, Kimanzichana mkoani Pwani, majambazi sita yakiwa na pikipiki tatu yalikivamia kituo cha polisi Mkamba, wilayani Mkuranga na kuua askari mmoja, mgambo wawili na kupora bunduki tano na risasi 60.
 
Vile vile Februari 3, mwaka 2015, Kilombero mkoani Morogoro, majambazi yalivamia na kuvunja ghala ya silaha kwenye kituo cha polisi Mgeta na kuiba silaha aina ya SMG na risasi 30.
 
Na machi 30, 2015, katika eneo la Kongowe jijini Dar es Salaam, majambazi yaliwavamia askari wawili kwenye kizuizi cha barabarani na kuwapora silaha mbili aina ya SMG, zenye risasi 60.
 
Aidha Mei 29, mwaka 2015, jijini Dar es salaam, majambazi walivamia lindo la askari wa kikosi cha Tazara na kupora silaha moja aina ya SMG.
 
Pia Julai 12 mwaka 2015, watu waliokuwa na silaha za moto walikivamia kituo cha polisi Stakishari, jijini Dar es Salaam, na kuua watu saba wakiwamo polisi. Aidha watu hao waliiba silaha 21, zikiwamo SMG 15 na SAR sita na risasi.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment