Wednesday, March 16, 2016

NAHODHA wa kikosi cha timu soka taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta ‘Popat’, anatarajiwa kuungana na kikosi cha timu hiyo nchini Chad, katika mchezo wa Stars dhidi ya Chad, Machi 23, jijini Djamena.

Samatta, anatarajiwa kuungana na kikosi hicho Machi 21, akitokea nchini Ubelgiji kwenye klabu yake ya (KRC) Koninklijke Racing Club Genk ya nchini humo.

Akizungumza na Mtembezi.com Mratibu wa timu ya taifa nchini, Msafiri Mgoyi alisema, hali ya Samatta kuuungana na timu nchini humo ni kutokana na ratiba jinsi ilivyowabana.

Alisema hata hapa nchini kikosi hicho kitaondoka kwa awamu tatu kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu katika timu zao za klabu ambazo zinacheza ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.

“Nahodha wetu (Samatta), tutakutana nae huko huko, tumeona iwe hivyo ni kutokana na ratiba jinsi ilivyotubana.

“Kundi la kwanza litaondoka nchini Machi 19, lingine litaenda Machi 20 na 21, unaweza kuona tunaondoka katika mazingira ya namna hii ni kutokana na ratiba yenyewe jinsi ilivyotubana.

“Yanga na Azam, zitakuwa na michezo yao ya kimataifa mwishoni mwa wiki hii, na timu za Simba na Mtibwa Sugar, zitakuwa na michezo ya ligi ya ndani, hivyo tutakuwa na muda mdogo mpaka kufikia siku ya mchezo wenyewe” alisema.

Mchezo wa marudiano wa timu hizo unatarajiwa kuchezwa Machi 28, katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Stars, inashika nafasi ya tatu katika kundi lake G, lenye timu za Misri ambao ndio vinara pamoja na timu za Nigeria na Chad.

0 comments:

Post a Comment