DAR ES SALAAM: Jeshi
la Polisi Tanzania kwenye viwanja vya ndege vilivyopo nchini limekuwa
likipambana na wauza madawa ya kulevya ‘unga’ kwa kugundua na kuzima
mbinu zote wanazotumia kusafirisha biashara hiyo haramu, hivyo kupunguza
kasi ya uingizwaji na utoaji wa unga kwa njia ya ndege, UWAZI
limeambiwa.
Akizungumza
na gazeti hii katika mahojiano maalum yaliyofanyika wiki iliyopita
Makao Makuu ya Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania yaliyopo jijini Dar,
Kamanda wa Viwanja vya Ndege, ACP Martin Otieno (pichani) alizitaja
mbinu kumi wanazotumia wauza unga hao kusafirishia bidhaa hiyo.
“Kwanza
napenda kuweka wazi kuwa, kwa sasa hatuna mchezo na wauza unga. Mbinu
zao zote wanazotumia kusafirishia madawa yao tunazijua. Na napenda
kuchukua nafasi hii kuwaambia wauza unga wote kwamba, hakuna atakayepona
safari hii,” alisema Otieno.
Akaendelea:
“Wamekuwa wakisafirisha unga kwa kuhifadhi ndani ya magogo. Gogo
linapasuliwa wanaweka unga humo. Barabarani askari wanajua ni magogo tu.
Wengine wanatumia vinyago. Wangine wanaingiza unga kwenye vipuli vya
magari.
Kamanda
Otieno akaendelea: “Lakini pia mbinu nyingine kubwa ni kuweka kwenye
sendozi za Kimasai. Wanaweka unga katikati ya soli na sehemu ya
kukanyagia, kisha wanashona. Wanapokaguliwa, wanasema ni sendozi
wanapeleka kuuza mikoani, kumbe katikati kuna unga. Pia wanatumia
hereni nene, kwenye soksi na bangili nene.
“Sasa
hivi kuna mbinu nyingine, wanachukua vitunguu, wanakata na kuondoa
nyama za katikati, wanaweka vipaketi vya unga, wanafunika. We ukiangalia
hivi unaona vitunguu.
“Pia
wapo wanaotumia sabuni za vipande, wanachimba katikati na kuweka unga
humo, wanavirudishia na kuviweka kwenye maboksi kama bidhaa
inayopelekwa kuuzwa kwa matumizi ya kufulia. Pia wengine wanatumia pindo
za suruali, wanaingiza unga katikati. Mbinu hizo na nyingine kibao
tunazijua, wasirogwe.
“Vigogo
hao wamekuwa wakijifanya wanasafirisha vitu hivyo wanavyofichia madawa
ya kulevya kama biashara lakini kutokana na ujuzi tulionazo pamoja na
vifaa na mbwa tumekuwa tukiwakamata. Nina uhakika kuwa biashara hii
inazidi kutoweka na ipo siku itakwisha kabisa.”
Kamanda
Otineo aliendelea kusema kuwa, ni kazi ngumu kupambana na wauza unga
kwani wamekuwa wakibuni mbinu kila kukicha lakini polisi na vyombo
vingine vya dola wamejipanga vizuri kuhakikisha hakuna anayepitisha
biashara hiyo katika viwanja vya ndege nchini.
Alisema
mafanikio mengine yanatokana na ushirikiano wa wananchi hivyo amewaomba
kuendelea kushirikiana kwani vita dhidi ya madawa ya kulevya siyo ya
serikali peke yake.
0 comments:
Post a Comment