"Kabla
sijaanza kuhutubia, naomba nimkaribishe mtu muhimu sana aliyefanikisha
ujenzi wa Daraja hili. Dkt Dau tafadhali karibu usalimie kidogo’’.
Ndivyo alivyoanza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli jana wakati wa uzinduzi wa daraja la kihistoria la
kigamboni alilopendekeza liitwe daraja la Nyerere kutukuza mchango wa
mwasisi wa taifa hili baba wa taifa hayati mwalimu Julius kambarage
nyerere.
"Watanzania wana tabia ya kusahau sana. Tunaweza kuzindua
hapa wakashangilia lakini wasiwapongeze watu waliofanikisha kazi
hiyo..mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”. Aliendelea Rais Magufuli mara
baada ya Dk. Dau kumaliza kusalimia.
Dk Magufuli alisema Balozi Dau
alimfuata ofisini kwake(wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi), akiwa
mnyonge na mwenye kukata tamaa ya kufanikisha mradi huo.
“Ndiyo
nikamwambia aanze kufanya kazi.” Rais Magufuli alisema ni Dk Dau na NSSF
ndiyo waliosimamia na kuhakikisha daraja hilo linajengwa na kukamilika
kwa kiwango hicho, akasema haitakuwa busara kulizindua bila kutambua
mchango wake.
Alisema ni kawaida kwa watu wenye michango mikubwa kusahaulika wakati wa mafanikio.
Tukio
hilo lilionyesha dhahiri kwamba Rais Magufuli amevutiwa kwa kiasi
kikubwa na kazi ya mkurugenzi huyo mstaafu wa NSSF na kwenda tofauti na
matarajio ya watu wengi waliokuwa na shauku ya kumsikia Rais
akimchukulia hatua mkurugenzi huyo kwa madai ya ubadhirifu wa mabilioni
ya fedha .
Hatua hii ya Rais kumwagia sifa hadharani Dk. Dau,
inakuja siku chache baada ya kusambazwa kwa kinachoitwa taarifa ya
mkaguzi wa hesabu za serikali CAG taarifa ambazo baadae zilikanushwa na
ofisi ya CAG .
Akizungumza
katika hafla hiyo, Dk Dau alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa
NSSF katika uwekezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Aliwakumbusha
Watanzania kumtanguliza Mungu akisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja
hilo kutasaidia kukuza uchumi na kurahisisha usafirishaji kwa wakazi wa
Kigamboni na Tanzania kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Rais
Magufuli alisema daraja hilo ni la kipekee katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati na kwamba litasaidia kukuza uchumi, utalii na ndiyo
maana hata majirani wanalitamani.
“Daraja hili linabeba zaidi ya tani elfu moja, ni daraja la kipekee, linao uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 100,” alisema .
Alisema
katika ujenzi wake uliofanyika kwa utaratibu wa PPP (Public Private
Partnership), Serikali imetoa asilimia 40 na NSSF asilimia 60 hivyo
vyombo vya usafiri kama baiskeli, guta, pikipiki na magari yatalipa
kuvuka.
“Leo hii, daraja hili limekamilika... halitambagua mtu
kwa sababu wa CCM watapita hapa wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri
mstahiki meya wa jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita
katika daraja hili… lakini wananchi waenda kwa miguu hawatalipia
matumizi ya daraja… ila wale waendesha baiskeli, pikipiki, maguta na
magari lazima walipie,” alisema Dk Magufuli.
Rais aliipongeza
kampuni ya China Railway Construction Engineering Group iliyotekeleza
mradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway Major Bridge
Group.
“Kwa kazi nzuri iliyofanywa na wenzetu hawa kutoka nchini
China napenda kutumia fursa hii kuahidi kwa niaba ya Serikali kuwa
tutaendeleza ushirikiano wetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
ikiwamo kumalizia kipande cha barabara kinachounganisha daraja hili
kutoka upande wa Kigamboni,’’ alisema.

0 comments:
Post a Comment