Saturday, April 16, 2016



NA IBRAHIM YAMOLA

KASHFA ya ufisadi inayolikabili Jeshi la Polisi ya kuingia mkataba na Kampuni ya Lugumi ya kufunga vifaa 108 vya kuhifadhi alama za vidole katika vituo vya polisi kwa gharama ya Sh. Bilioni 37,
imegeuka shubiri kwa vigogo na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, aliyejitokeza kujibu kuhusu uhusiano wake na kampuni hiyo. Jeshi la Polisi liliingia mkataba na kampuni hiyo mwaka 2011 na limelipa asilimia 99 ya fedha walizotakiwa kulipa, lakini hadi sasa wamepatiwa mashine 14 na kati ya hizo mbili tu ndizo zinazofanya kazi.
 

Ridhiwani ambaye katika utawala wa baba yake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, unaolaumiwa kwa kufumbia macho uzembe, ubadhirifu na ufujaji wa mali za umma, alikuwa akihusishwa na kufanya biashara mbalimbali hapa nchini ingawa mara kadhaa alizikana tuhuma husika, amekuwa mtu wa kwanza kuzungumzia kashfa hiyo.
 

Kashfa hiyo iliibuliwa wiki iliyopita na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ikihusisha vigogo wa serikali. Vigogo wanaohusihwa kwenye kashfa hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, anayetajwa kujihusisha kibiashara na mmiliki wa Kampuni ya Lugumi, Said Lugumi, ambaye inamwelezea kuwa ni baba mkwe wake. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba, ambao wawili hao wanadaiwa Kampuni yao ya Infosys ilishirikiana na ya Lugumi kufunga mashine hizo.
Kitwanga na Kipilimba wanadaiwa kuanzisha kampuni hiyo wakiwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 

Katika tuhuma ambayo Jeshi la Polisi inalikabili ni baada ya kuingia mkataba mwaka 2011 na Kampuni ya Lugumi ya kufunga vifaa 108 vya kuhifadhi alama za vidole katika vituo vya polisi kwa gharama ya Sh. Bilioni 37, lakini malipo yamefanyika kwa asilimia 99 huku mashine zinazofanya kazi ni mbili pekee.
Utata mwingine ambao unaibua maswali mengi unatokana na ukubwa wa gharama ya Sh. Bilioni 37, sawa na Sh. Milioni 342 kwa mashine moja.
 

Kujitokeza kwa Ridhiwani kuzungumzia tuhuma hizo ni baada ya taarifa kusambaa mitandaoni zikimtaja kuwa mmoja wa wanaoshirikiana na Kampuni ya Lugumi pamoja na Mwema. Ridhiwani ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze (CCM), mkoani Pwani, wakati mkataba huo unasainiwa mwaka 2011 kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi, baba yake, Rais mstaafu Kikwete alikuwa Rais, huku Said Mwema alikuwa IGP.
 

Tuhuma za sakata hilo ziliibuka baada ya watendaji wa Jeshi la Polisi kufika mbele ya PAC wiki iliyopita, ambapo maelezo kuhusu mkataba huo yaliwachanganya wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe hao walishindwa kuelewa, hasa kutokana na kwamba ni mashine 14 pekee kati ya 108 ndizo zimefungwa huku Kampuni ya Lugumi ikiwa imekwisha kulipwa asilimia 99 ya Sh. Bilioni 37 ambazo ni Sh. Bilioni 34.
 

Kutokana na utata huo, PAC imewapa siku sita watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa inayoelezea mchanganuo wa mkataba huo ambapo siku hizo zilizotolewa zinatimu kesho.
Maelezo ya Ridhiwani Tanzania Daima Jumapili lilimtafuta Ridhiwani juzi, ambaye alikuwa akihudhuria vikao vya Kamati ya Bunge akiwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo, hasa likitaka kufahamu anazungumziaje taarifa zinazosambaa katika mitandao zikimhusisha yeye na kashfa hiyo, ambapo alisema:
“Hivi unataka kuniambia kuna kitu gani kingine ambacho mnataka kuandika zaidi ya kile mlichoandika leo (juzi)?” alihoji Ridhiwani.
 

Habari ambayo Ridhiwani alikuwa anaizungumzia iliyoandikwa na gazeti hili juzi ilihusu kashfa hiyo ikiwa na kichwa cha habari ‘Mtoto wa Rais mstaafu matatani’, lakini haikumtaja jina na lilimweleza katika mitandao unatajwa moja kwa moja je, unazungumziaje tuhuma hizo? Ridhiwani alisema: “Siwezi kuzungumzia suala hilo.” Lakini, Ridhiwani akizungumza na moja ya gazeti la kila siku (si gazeti hili) alikanusha taarifa hizo zilizosambaa mitandaoni zikimhusisha yeye na Kampuni ya Lugumi.
 

Alisema yeye hahusiki na kampuni yoyote ya Lugumi ingawa alikiri kwamba wana urafiki wa kawaida na mmiliki wa kampuni hiyo, Said Lugumi, na wala hafahamu ni kwa nini amehusishwa na Kampuni ya Lugumi.
“Mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la msingi kabisa, watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye na ni rafiki yangu,” alinukuriwa na gazeti hilo na kuongeza:
 

“Hapa ni watu tu wanaamua kuingiza tu maneno yao, haya maghorofa ninayotajwa kumiliki Dar es Salaam hata sijawahi kutembelea ujenzi wake, wameamua kuniingiza, Lugumi nafahamiana naye binafsi tu lakini wananiingiza,” alisema Ridhiwani.  Alisema jambo hilo bado limo ndani ya Kamati ya Bunge na baadaye ameliona kwenye magazeti ya juzi kuwa Jeshi la Polisi litatoa taarifa yao, hivyo asingependa kulizungumzia kwa undani. Mtoto huyo wa rais mstaafu alisisitiza kwamba angependa jamii ifahamu kuwa hana uhusiano na kampuni hiyo kwa kuwa hafahamu kabisa hata malipo yaliyofanywa kati ya serikali na Kampuni ya Lugumi, anasikia tu kama ambavyo watu wengine wamesikia.
Mwema

IGP mstaafu, Said Mwema, akizungumza na Tanzania Daima Jumapili kuhusu kuhusishwa kwake na Kampuni ya Lugumi na kashfa iliyotokea akiwa Mkuu wa jeshi hilo, alisema IGP ni ofisi, siyo mtu binafsi na jukumu hilo la U- IGP alikwisha likabidhi kwa mtu mwingine. “Kama nitatakiwa mimi binafsi kutoa ufafanuzi nitatoa majibu na kama majibu au maswali yatahusu ofisi, basi ninaomba muwasiliane na waliopo ofisini, kwani IGP ni ofisi,” alisema Mwema. Tanzania Daima Jumapili lilitaka kujua taarifa ambazo zinasambaa mitandaoni zikimhusisha yeye na Lugumi katika kashfa hiyo alisema: “Kwa hilo ninaomba muwaulize hao ambao wanasambaza hizo taarifa, watoe ushahidi, kwani mimi nashindwa nizungumze nini.”
 

Mwema alinukuu hotuba ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba: “…Mwalimu Nyerere aliwahi kuuliza swali ambalo kuna watu hawakulipenda kwamba kila unayemuita baba ina maana amemuoa mama yako? Kila mtu anaweza kusema anavyoona inafaa. “Hao wanaosema waweke ushahidi na kama tutatakiwa kuhojiwa tutahojiwa na tutajibu…kama alimwoa mtoto wangu, waonyeshe hata ushahidi wa picha, kwani,” aliongeza.
 

Mara baada ya kauli hiyo, Tanzania Daima Jumapili lilirejea swali, hasa likitaka kufahamu kama aliwahi kujihusisha na Lugumi katika masuala ya kibiashara ambapo alisema: “Wao wanasema, watoe vielelezo lakini kama nilivyosema kauli aliyoitoa Mwalimu Nyerere.” Alipoelezwa ni hatua gani anakusudia kuzichukua kwani kama hajihusishi na biashara pamoja na Lugumi na mwenzake Ridhiwani amejitokeza na kukanusha, yeye alisema: “Hapa najizungumzia mimi, labda wewe (anamweleza mwandishi) afadhali umeona nachafuliwa, ungenishauri nifanye nini sasa?”
Kipilimba, Kitwanga wafunguka

Kipilimba alisema: “Mimi sijawahi kuunda au kumiliki kampuni hiyo (Infosys), siijui hata mkienda Brela na sijawahi kujihusisha na kampuni hiyo.” Tanzania Daima Jumapili lilimuuliza Kipilimba kama anaifahamu kampuni hiyo, ambapo alisema: “Mimi simo kabisa, ila kampuni ipo, naijua, ila sijawahi kuifuatilia.”
Naye Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Misungwi (CCM), mkoani Mwanza alipopigiwa simu yake ya kiganjani akiwa mkoani humo, hakupokea, lakini alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ukimweelza kwamba kuna taarifa zinamhusisha na Kampuni ya Infosys kama anaifahamu. Waziri huyo alijibu ujumbe huo kwa ujumbe mfupi wa maandishi akisema: “Hayo maneno yako, pata ukweli.” Tanzania Daima Jumapili baada ya kupokea ujumbe huo, lilimweleza Kitangwa kwamba: “Ndiyo maana tunaomba kupata ukweli.”
Baada ya muda, Kitwanga alipiga simu na kusema: “Ninyi waandishi fanyeni research (utafiti) kwanza ili kupata ukweli na msilopokelopoke tu.”
 

Mara baada ya kauli hiyo, Tanzania Daima Jumapili lilimuuliza huo ukweli ambao anauzungumzia ni upi na ghafla alikata simu na alipotafutwa tena hakupokea simu wala kujibu ujumbe aliotumiwa kuhusu kampuni hiyo.Utata wa mashine hizo Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili umebaini kwamba mashine hizo zilizofungwa mwaka 2011 na Kampuni ya Lugumi ni aina ya Automaded Finger Print Information System (AFIS), zilizofungwa nchi nzima lakini ni mashine mbili tu ndizo zinazofanya kazi.
Kigogo mmoja wa Polisi aliyezungumza na gazeti hili juzi na kuomba hifadhi ya jina lake, alisema:
 

“Hizo mashine zote ni mbovu, isipokuwa ni mbili tu ndizo zinafanya kazi, ambazo zipo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Msimbazi, jijini Dar es Salaam.”  Alisema tatizo la mashine hizo hata wataalamu wa kuziendesha ni wachache na kama taratibu za sheria za manunuzi zingefuatwa, zisingenunuliwa au kufungwa.
“Mimi nazungumza ninajua, nilikuwa makao makuu lakini mashine za AFIS wakati zinapekekwa pale, kwanza zilipelekwa kwa amri maalumu kutoka kwa mkuu (Said Mwema) na ilikuwa lazima zifungwe na kuanza kufanya kazi mara moja,” alidokeza na kuongeza: “Ilileta tafrani, kwani hata wataalamu wa kuzitumia hawakuwapo, lakini walikuja Wazungu kutoka Ujerumani na wengine sijui wapi na kuwafundisha vijana wa IT kwa wiki mbili na wakaondoka.” Alisema baada ya kuondoka, vijana wale walianza kulalamika kwamba wamefundishwa kuzitumia, lakini hawajapewa mafunzo ya jinsi ya kuzitengeneza zitakapoharibika.
“Wakati huo Lugumi alikuwa amepelekewa fedha yake na taarifa ilitakiwa itolewe haraka kwamba zinafanya kazi na vijana wale walishindwa kugoma kwani amri ilitoka kwa kigogo wa polisi, hivyo wasingeweza kukataa,” alisema na kuongeza:
 

“Baada ya minong’ono kuongezeka ndipo vijana hao wakatakiwa kwenda kuzifunga mashine hizo nchi nzima lakini ninapozungumza nawe kama nilivyosema ni mashine mbili tu zinafanya kazi, zingine majanga,” alisema.
Kuhusu malipo ya mashine hizo alisema: “Fedha za malipo zilikuwa zinatoka moja kwa moja Hazina na zilielekezwa alipwe Lugumi, sasa tukabaki tunajiuliza, kwa nini fedha zinatoka Hazina na kuelekezwa moja kwa moja zilipwe kwa Lugumi badala ya fedha hizo kuachwa zipangiwe na wizara?”

IGP Mangu

Juzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, aliyepokea mikoba ya Mwema akizungumzia sakata la mashine hizo alisema: “Mashine zote zilizofungwa nchi nzima zinafanya kazi.”
Alipoulizwa kuhusu kauli ya PAC kwamba mashine 14 ndizo zilizofungwa, tena jijini Dar es Salaam tu, alisema: “Siyo kweli, watu wana maugomvi yao, lakini nakueleza kwamba mashine zimefungwa nchi nzima na kama hawaamini waende wakakague na huko watazikuta, mbona hakuna tatizo.
 

“Tatizo jingine hazifanyi kazi kwa kukosa kuunganishwa na mtandao wa intaneti, kwani tumekatiwa mawasiliano na TTCL wanatudai na hapa Dar es Salaam zinafanya kazi kwa kuwa tumeunganishwa na Mkongo wa Taifa,” aliongeza.
 

Alipoulizwa ni kiasi gani ambacho TTCL wanalidai Jeshi la Polisi, alisema: “Hilo sasa ni suala la ndani, lakini kama hamuamini nendeni TTCL mkaulize watawaeleza wanatudai kiasi gani.”
Alisisitiza kuwa kama watu wamepanga kuwachafua, waendelee lakini mashine hizo zimefungwa nchi nzima na zinafanya kazi.


Chanzo:Gazeti La Tanzania Daima, 10/4/2016.

0 comments:

Post a Comment