Rais John Magufuli amemteua Mathias Chikawe kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.
Huu
ni mwendelezo wa kuwakumbuka kwa kuwapangia majukumu ya kitaifa baadhi
ya makada wa CCM waliopambana naye katika mbio za kuwania nafasi ya
urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kabla
ya kupangiwa kituo hicho cha kazi, Chikawe aliteuliwa kuwa balozi
Februari 15, mwaka huu sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Hifadhi wa Taifa (NSSF), Dk Ramadhani Dau na Dk Asha-Rose Migiro.
Chikawe,
ambaye ameanza kutekeleza majukumu yale tangu Aprili 13, alikuwa
miongoni mwa makada 38 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu za kuwania
nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM.
Makada waliokumbukwa
Makada
wengine waliokumbukwa katika Serikali ya Magufuli ni Profesa Sospeter
Muhongo, Dk Harrison Mwakyembe, January Makamba, Mwigulu Nchemba, Dk
Khamis Kigwangalla, Balozi Augustino Mahiga na Dk Asha-Rose Migiro.
Ukimuondoa
Dk Migiro anayesubiri kupangiwa kituo cha kazi baada ya awali kuteuliwa
kuwa balozi, waliobaki kwa sasa wanamsaidia Rais baada ya kuwateua kuwa
mawaziri.
Baada ya kuapishwa, Rais Magufuli, alimteua Dk Mahiga
kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kitaifa.
Dk Mwakyembe, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria. Akamteua Makamba kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano
na Mazingira.
Wengine ni Luhaga Mpina aliyemteua kuwa Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Khamis
Kigwangwalla (Naibu Waziri Afya, Maendeleo, Jinsia, Wazee na Watoto),
Mwigulu Nchemba (Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi). Rais Magufuli
alimteua pia Profesa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Makada visiwani
Kwa
upande wa visiwani Zanzibar, makada waliopambana na Magufuli kupitia
CCM na wameteuliwa na Rais Ali Mohamed Shein kushika nafasi za uongozi
kwenye Serikali yake ni Balozi Amina Salum Ali na Balozi Ali Karume,
ambao wote waligombea nafasi za urais wa Tanzania.
Akitoa maoni
yake kuhusu uteuzi wa Magufuli, mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally
Kessy alisema: “Kugombea nafasi kama hiyo siyo kuwa maadui, mbona hata
Rais mstaafu Kikwete (Jakaya) aliwahi kufanya hivyo,”alisema.
Mwingine
aliyeunga mkono hatua ya Rais ni mwanasheria maarufu nchini, Profesa
Abdallah Safari aliyesema Rais ana haki ya kumteua mtu yeyote anayemuona
anaweza kumsaidia katika uongozi.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:
Post a Comment