MWIGULU Nchemba Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameomboleza msiba
wa Christina Mughwai, mbunge wa zamani wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) mkoa wa Singida, na kumsifu marehemu kuwa alikuwa
mzalendo aliyetanguliza maslahi ya taifa mbele katika ubunge wake, Anaandika Josephat Isango.
Nchemba ameyasema hayo leo mchana, baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach, barabara ya Bagamoyo mtaa wa Makonde alipofika kusalimia ndugu pamoja na waombolezaji.
Alitumia fursa hiyo kukaa na wanafamilia na ndugu waliohudhuria hapo
kabla ya kutoa maneno machache kwa jinsi anavyomfahamu marehemu
Christina.
“Msiba hauna itikadi za vyama, msiba unatuhusu wote, na hawa ni ndugu
zangu toka Singida, na huyu marehemu ni mtu wangu wa karibu nimefanya
naye kazi kwenye kamati ya bajeti, yeye akiwa naibu msemaji wa Wizara ya
eEdha, kweli ni mtu makini aliyetanguliza maslahi ya taifa badala ya
maslahi binafsi.” Alisema Mwigulu
Aliongeza kwamba, marehemu alikuwa ni mtu anayeweza kushauri ukweli
na ushauri mzuri hivyo kifo chake ni pengo kwa taifa, kwa chama chake na
watu wa Singida ambao amewatumikia kwa miaka mitano kwa nafasi yake ya
Ubunge wa viti maalumu.
Tofauti na ilivyotarajiwa kwa sababu za utani wa Wanyiramba (kabila
la Mwigulu) na Wanyaturu (Kabila la Lissu), Mwigulu alikuwa mstaarabu
hakuingiza utani kwenye msiba kama ilivyozoeleka kwa makabila
yanayotaniana humu nchini.
Alitumia muda mrefu kuongea na dada mkubwa wa Lissu ( Mama Kabula)
kabla ya kukaa na wazee, kuwapa pole, kutoa rambirambi na kuwaaga.
Wakizungumza baada ya kuondoka kwa Waziri huyo, baadhi ya Wazee
kutoka Singida walimsifu kwani wamekuwa wakihasimiana bungeni lakini
kwenye suala la msiba, ameonyesha hakuna itikadi za vyama na
ameshirikiana na ndugu zake toka Singida, jambo waliloita ni ukomavu wa
siasa.
Christina, amefariki dunia Aprili 8 mwaka huu, anatarajiwa kuagwa
katika viwanja vya Karemjee, Jumanne, Aprili 12 na kuzikwa nyumbani kwao
wilaya ya Ikungi Aprili 13, siku ya Jumatano.

0 comments:
Post a Comment