Sunday, May 15, 2016


Dar es Salaam. Rufaa ya kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Tigo dhidi ya wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hamisi Mwinyijuma ‘Mwana FA’ na Ambwene Yesaya ‘AY’ ya kuzuia isiwalipe Sh2 bilioni kwa kuvunja sheria ya hakimiliki imekwaa kigingi, baada ya kuwekewa pingamizi.

Tigo imefungua maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikiomba kusimamisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliyoiamuru kuwalipa fidia wasanii hao, baada ya kuishtaki kwa kukiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kutokana na kutumia kazi zao bila ridhaa wala makubaliano nao.

Kazi hizo ambazo kampuni hiyo ilizitumia bila ridhaa wala makubaliano ni wimbo uitwao Usije mjini wa MwanaFA na Dakika moja wa AY.

Kutokana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Ilala, Tigo imekata rufaa Mahakama Kuu kuipinga.

Sambamba na rufaa hiyo, kampuni hiyo imefungua maombi ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo hadi rufaa yao itakapotolewa uamuzi.

Hata hivyo, wasanii hao wanaowakilishwa na Wakili Albert Msando waliiwekea pingamizi la awali kampuni hiyo dhidi ya maombi hayo ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo, wakiiomba Mahakama Kuu iyatupilie mbali.

Pingamizi la wasanii hao dhidi ya maombi hayo ya Tigo lilisikilizwa juzi na Jaji Isaya Arufani na wasanii hao kupitia kwa Wakili wao, Msando waliwasilisha hoja tatu za kupinga maombi hayo.

Baada ya kusikiliza hoja za pingamizi la wasanii hao pamoja na majibu ya Tigo kupitia kwa Wakili wake, Rosan Mbwambo, Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi mwezi ujao itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya usikilizwaji wa pingamizi hilo, Msando alisema iwapo Mahakama katika uamuzi wake itakubaliana na hoja za pingamizi lao na kutupilia mbali maombi hayo, wataendelea na utekelezaji wa hukumu hiyo, licha ya kukatiwa rufaa.

Awali, Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Ilala, Juma Hassan alitoa hukumu ya kesi hiyo Aprili 11, akiwapa ushindi wasanii hao maarufu wa Bongo Fleva.

0 comments:

Post a Comment