Katika
matukio yote yaliyorekodiwa nchini katika kipindi cha mwezi mmoja
uliopita, watu wasiojulikana wamekuwa wakitumia silaha kama visu,
mapanga, na mashoka baadhi wakiwa na alama za kundi la IS.
Matukio
yaliyotikisa nchi ni ya watu saba wa familia moja katika kijiji cha
Sima Wilaya ya Sengerema kuchinjwa; watu watatu kuuawa katika msikiti wa
Rahman Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani; na kuuawa Mwenyekiti wa kijiji
cha Bulale Kata ya Buhongwa pia Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Mauaji mengine yaliyoishtua nchi ni ya watu wanane katika eneo la
mapango ya Amboni, Tanga.
Ili
kuhakikisha wahalifu wanapatikana wakiwa hai au wafu, Jeshi la Polisi
lililazimika kutumia silaha nzito za kivita kukabiliana nao. Polisi
hawajafanikiwa kukamata wauaji wa watu wanane Tanga, lakini usiku wa
kuamkia Jumapili, Polisi mkoani Mwanza walifanikiwa kuvamia mapango
yaliyoko katika mlima wa mawe Utemini na kuwaua watuhumiwa watatu wa
uhalifu.
Akizungumzia
tukio la Amboni, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Abdullah Luhavi alisema majibu
yote yatapatikana baada ya oparesheni na akashauri vyombo vya ulinzi
viachwe vifanye kazi yake.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akielezea mafanikio ya mapambano
katika mapango ya Utemini alisema mkakati wa Serikali wa kufanya Mwanza
kuwa sehemu salama umeanza na hakutakuwa na mhalifu atakayeingia na
kutoka salama.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema jeshi hilo linaendelea na
kazi yake na kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu
alishazungumzia mauaji hayo akiwa Tanga. “Tutatoa taarifa tena baadaye
lakini kwa sasa tayari IGP alishazungumza,” alisema.
Maswali
Wananchi
wanahoji maswali kadhaa jinsi matukio ya Mwanza na Tanga yanavyofanana
kwa muda wa uhalifu, sababu, namna mauaji yanavyofanyika, vifaa vya
uhalifu, wanakojificha na silaha zinazotumiwa na Jeshi la Polisi
kupambana na wahalifu hao.
Kwa nini mauaji ya Tanga na Mwanza yalitokea baada ya watoto kukamatwa?
Katika
tukio la Tanga, mke wa marehemu Mkola Said, Asha Said alisema wauaji
walipofika nyumbani kwake walimuuliza mumewe: “Wako wapi watoto wetu
mliowapigia simu polisi wakawachukua?”
Ilidaiwa
kuwa siku chache kabla ya tukio hilo watoto nane wenye umri wa kati ya
miaka 10 hadi 16 walipita kijijini hapo na kukamatwa, ingawa moja
alikimbia.
Pia,
mauaji ya watu watatu katika msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini akiwamo
imamu Feruz Ismail yaliyofanyika Mei 18 ni baada ya watoto kukamatwa.
Ilidaiwa siku chache kabla ya mauaji hayo, polisi walivamia na
kuwakamata vijana kadhaa waliokuwa wakifanya mafunzo ya karate katika
moja ya misikiti mitatu iliyoko Utemini.
Mmoja
wa mashuhuda wa tukio hilo alisema wauaji hao walikuwa wameshika
bendera nyekundu iliyokuwa na maandishi meupe yaliyosomeka IS. Kadhalika
shuhuda huyo alieleza kuwa kabla ya kuua walimuuliza Imamu:
Mfano huu wa tukio la Mwanza na la Tanga umezua maswali kwamba huenda wauaji hao ni wale wale au wenye lengo moja.
Kwa nini mauaji ya kuchinja yalifanyika saa 7.00 usiku?
Matukio
mawili ya mauaji yalifanyika muda wa saa saba usiku. Tukio la kwanza
lilitokea Mei 10 katika kijiji cha Sima Wilaya ya Sengerema mkoani
Mwanza, ambako watu saba wa familia moja waliuwawa kwa kukatwa mapanga.
Tukio linalofanana na hilo ni la mauaji ya watu wanane yaliyofanyika Amboni, Tanga Mei 28.
Kwa nini wamelenga viongozi?
Japokuwa
hadi sasa haijulikani kwa dhati sababu za vifo vya watu hao, wauaji wa
Amboni Tanga walilenga viongozi waliotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi
kwenda kuwakamata watoto waliopita katika eneo hilo; mauaji ya Imamu
Feruzi kwa madai ya kuendelea na ibada wakati wenzao wamekamatwa na pia
aliuawa Mwenyekiti wa Bulale alipokuwa akisuluhisha wanandoa.
Kwanini wauaji wanajificha kwenye mapango?
Mara
kwa mara wahalifu wanaofanya uhalifu Tanga, hukimbilia kujificha katika
mapango ya Amboni na walioua waumini msikitini Mwanza walikwenda
kujificha katika mapango jirani katika eneo la mlima wa mawe Ibanda
Relini. Je, kuna usalama wowote katika mapango mengine nchini. Ni swali
ambalo hakuna ofisa yeyote aliyekuwa tayari kujibu jana.
Kwa nini polisi walipambana na majambazi hayo kwa zaidi ya saa 14?
Katika
mapambano dhidi ya wanaoitwa majambazi kule Amboni, polisi
hawajafanikiwa kumkamata yeyote; mwaka jana mwanajeshi mmoja aliuawa,
lakini hakuna jambazi aliyenaswa. Katika eneo la Utemini polisi
wamepambana na kufanikiwa kuwaua watatu baada ya zaidi ya saa 14. Je,
hao ni majambazi wa kawaida?
Kwa nini polisi wanatumia silaha za kivita?
Jeshi
la Polisi mara zote huwa linadai linakabiliana na wahalifu wa kawaida,
majambazi na vibaka lakini kinachowashtua watu ni matumizi ya silaha
nzito za RPG za kudungulia ndege au kuharibu vifaru. Watu wanahisi
wahalifu hao si wa kawaida na hapo kunazua maswali zaidi.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba
alisema kiuhalisia mauaji hayo yanatisha na kwamba yameleta sura
tofauti.
“Wananchi
wanachanganyikiwa na kujiuliza maswali mengi kwamba, mauaji haya ni
ugaidi? Kiukweli mauaji haya yamesababisha taharuki kubwa miongoni mwa
jamii,”alisema.
Alisema
ipo haja kwa vikosi vyote vya usalama kuimarisha usalama wa raia na
mali zao ili kuwanusuru na mauaji yanayoendelea kutokea wakati, vikosi
hivyo vipo.
Makamu
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole-Sosopi
alisema ni jukumu la Serikali kutoa majibu ikiwa matukio hayo ni ya
kigaidi au la ili kuondoa hofu kwa jamii. “Inaogofya na kutisha kwa
sababu bado tuna wasiwasi juu ya mauaji haya. Serikali ilikaa kimya hadi
ilipoona matukio yanazidi kuwa makubwa. Tunachotarajia ni majibu
yatakayosaidia kuwafanya wananchi watulie, kwa sasa bado kuna
hofu,”alisema.
Sosopi pia alisema Serikali inatakiwa kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuwezesha kazi za ulinzi.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kwa kuwa matukio
hayo huwa ni ya msimu, lazima suala la ulinzi na usalama wa raia
liimarishwe.
“Siyo
mara ya kwanza kwa Amboni kutokea mauaji haya, ni vizuri kuanzishwe
kikosi cha jeshi ili kuwahakikishia usalama raia walioingiwa na
hofu,”alisema.
Mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM, Frank John alisema licha ya kuwa matukio hayo
yanatisha, bado jamii haipaswi kukwepa jukumu la kusaidia ulinzi na
usalama kwenye eneo lake, ikiwamo kutoa taarifa ya wageni wanaoingia na
kutoka.
Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo,
amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha vitengo vya
intelijensia ili kukabiliana na uhalifu wa kimakundi. “Mambo haya
yanayoendelea nchini tujue kuwa jamii yetu imeingia katika hali ambayo
inatishia usalama wa wote si waislamu, wakristo au madhehebu mengine.
Tuvisaidie vyombo vyetu,”alisisitiza.
Juzi,
Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zuberi aliitaka Serikali kuhakikisha
inalinda amani na alilaani mauaji yanayoendelea nchini.
Imeandikwa na Tumaini Msowoya na Burhani Yakub.
0 comments:
Post a Comment