MWANZA:
Muuza duka la dawa baridi ‘famasi’ katika Kijiji cha Matara wilayani
Kwimba, Stephen Ng’wanyi anasakwa na jeshi la polisi akituhumiwa
kusababisha kifo cha Anna Martine (18) baada ya kudaiwa kumdunga sindano
kwa lengo la kumtoa mimba.
Anna
alidaiwa kufariki dunia Julai 20, mwaka huu majira ya 2:00 asubuhi,
baada ya kudungwa sindano na muuza duka huyo ili kutoa ujauzito wa miezi
mitatu aliokuwa nao.
Ilielezwa
kuwa Julai 19, marehemu alikuwa akilalamika kuumwa tumbo kutwa nzima
lakini kutokana na maumivu kuzidi aliamua kumweleza dada yake Anna
Fabian kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na alidungwa sindano ya
kuutoa huku akimtaja Stephen Ng’wanyi.
Hali
yake ilizidi kuwa mbaya na kusababisha dada yake marehemu kwenda
kumwita Ng’wanyi ili aje kumpa matibabu mdogo wake nyumbani hapo, lakini
baada ya kufika aliwashauri ndugu wa marehemu aondoke naye hadi
nyumbani kwake kwa matibabu zaidi.
Kutokana
na maombi hayo ndugu waliridhia Ng’wanyi kuondoka na Anna hadi kwake na
muda mfupi baadaye alirejea na kuwaeleza ndugu hao kuwa mgonjwa
alifariki dunia na baada ya kuwaambia alitoroka.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Augustino Senga alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi hilo linamsaka muuza duka
huyo kwa udi na uvumba ili afikishwe mahakamani kwa kosa la mauaji.
“Jeshi
la polisi lipo kwenye msako kuhakikisha linamkamata mtuhumiwa huyo
anayedaiwa kusababisha kifo cha Anna na kumfikisha mahakamani ingawa
upelelezi unaendelea na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Magu kwa uchunguzi,” alisema Senga.
Kaimu
kamanda huyo wa polisi alitoa onyo kwa wananchi wa Jiji la Mwanza hasa
wasichana, kuwa kutoa mimba bila sababu za kitabibu ni kosa la jinai na
kinyume cha sheria na kuwashauri kutofanya hivyo.
Pia
aliwataka wamiliki na wauzaji wa maduka ya dawa baridi wafanye biashara
hiyo kwa kuzingatia taaluma yao na kwa mujibu wa masharti ya leseni zao
yanavyoelekeza na si vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment